SERENGETI BOYS YAPAA, MCHAWI MWEUSI ATAMBA
Timu ya Taifa ya
Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeondoka saa 9.45 alfajiri
ya leo Juni 30, 2016 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwenda Visiwa va
Hame-Shelisheli kwa ajili ya kuwavaa wenyeji katika mchezo wa marudiano kuwania
nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.
Serengeti Boys
inaondoka na matumaini makubwa ya kuiondoa Shelisheli katika mbio hizo baada ya
kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, Jumapili ya Juni 26, 2016. Ili ifuzu, Serengeti Boys
inahitaji kusimama imara katika matokeo hayo ama kwa kupata sare ya aina
yoyote, kushinda au ikitokea kupoteza, basi isifungwe zaidi ya mabao 2-0.
Lakini Kocha
Mkuu wa vijana hao, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi kutoka Tanga, amesema,
“Nawaheshimu Shelisheli, lakini vijana wangu hawawezi kuwapa nafasi hata kidogo
wapinzani wetu. Hapa tulishinda, na kwako tunakokwenda tunakwenda kushinda.
Vijana wangu wa Serengeti Boys wako vizuri. Nawapenda na wao wanatupenda
makocha wao na viongozi wote wa TFF.”
Katika mchezo wa
Dar es Salaam waliozifumania nyavu walikuwa Nickson Kibabage, Ibrahim Abdallah
na Ally Hussein ambaye alifunga ambao kila mmoja amepania kufunga kama kocha
akiwapa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza kwa sababu Mchawi Mweusi
amefunga safari hiyo akiwa na kikosi cha nyota 20 wa timu hiyo inayolelewa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Jamal Malinzi.
Nyota
waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili na Samwel Edward Brazio
wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel
Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.
Viungo ni Kelvin
Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor
Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Yassin Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku
washambuliaji wakiwa ni Rashid Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah Rashid,
Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima Makame na Enrick Vitalis Nkosi.
Serengeti Boys ambayo
haina mdhamini badala yake ikihudumiwa na TFF yenyewe ilikuwa kambini tangu
Juni 14, 2016 kujiandaa na mechi hizo za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika dhidi ya Shelisheli na Afrika Kusini ambayo itapambana nayo baadaye
mwezi ujao.
Katika kuajindaa
na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki
mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International
Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika
Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya
Korea Kusini na Marekani.
…………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA
Post a Comment