SINGIDA UNITED WASIKITISHWA NA MAAMUZI YA ALLIANCE ACADEMY

Na Said Ally
Uongozi wa klabu ya Singida United umesema kwamba haujapokea malalamiko yoyote kutoka katika klabu ya Alliance ya jijini Mwanza kuhusiana na swala la usajili wa mchezaji Ally Ng'anzi aliyesajiliwa na klabu hiyo ya Singida katika dirisha dogo.

Mkurugenzi wa klabu ya Singida United Festus Sanga alisema kwamba uongozi wa klabu hiyo umesikitishwa na kitendo kilichofanywa na klabu ya Alliance kutoa malalamiko yao katika vyombo vya habari wakieleza kuwa Singida United ilimsajili mchezaji wao Ally Ng'anzi pasipo kufuata taratibu za usajili.

Sanga alisema kwamba uongozi wa Singida United ulifanya usajili wa mchezaji huyo kupitia wakala wake Stephano Mkomola ambao wote kwa pamoja hawakueleza kama mchezaji huyo angali anamilikiwa na timu nyingine.

Alisema kwamba uongozi wa Singida United uko tayari kufanya mazungumzo na Alliance ili kupata muafaka kamili kama wanaamini mchezaji ni wao kwani huenda labda mchezaji na wakala wake walidanganya kuhusiana na kutokuwa na mkataba na klabu nyingine.

Aidha alisema kwamba endapo kama kutabainika mchezaji ni wao, Singida United haitasita kumuachia kuendelea kuitumikia timu hiyo endapo kama hawataafikiana muafaka kamili.

Hata hivyo Sanga aliongeza kusema kuwa lengo la klabu ya Singida United ni kukuza vipaji vya vijana ambao watakuwa na faida kubwa kwa timu na Taifa kwa ujumla hapo baadae na ndio maana wakaamua kuwapa mikataba wachezaji wanne kutoka timu ya vijana ya Serengeti Boys akiwemo Ng'anzi ili kupata uzoefu wakiwa na klabu hiyo.

No comments