MIAKA 21 YA LIGI YA MUUNGANO. MIAKA 15 BILA LIGI YA MUUNGANO

NA PASCAL KABOMBE
Ligi ya Muungano ilianza rasmi mwaka 1982 lengo ni kudumisha Muungano wetu na kutoa usawa wa kiuwakilishi katika michuano ya kimataifa ya vilabu, hii ni kutokana na Tanzania bara kuwa na ligi yake na Zanzibar kuwa na ligi yake huku upande wa pili (Zanzibar) ukiwa sio mwanachama wa shirikisho la soka barani Africa caf, hivyo kukosa sifa ya timu zake kushiriki michuano ya vilabu bingwa africa na kombe la washindi (ilijulikana hivyo miaka hiyo). Kwa kuwepo kwa ligi ya Muungano ambayo ilikuwa inajumlisha timu 3 zilizomaliza nafasi juu kwenye ligi husika basi timu kutoka Zanzibar nazo zilipata nafasi ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano kwenye michuano ya CAF. Moja ya timu iliyofanya vizuri sana kimataifa katika uhai wa miaka 21 ya michuano hiyo kwa upande wa Zanzibar ni timu ya Malindi (nitaelezea kwa utuo katika makala nyingine kuhusu vilabu vya Zanzibar na michuano ya kimataifa). 

MIAKA 21. 

Michuano hii ilifanyika kwa miaka 21 mfululizo na ikishuhudia timu 9 zikiibuka na kombe hilo katika miaka tofauti tofauti. Pamoja na kwamba ligi hiyo ilikuwa na timu 6 kila mwaka bado ni hizo timu 9 tu ndio ziliibuka kidedea kila mmoja kwa wakati wake, baadhi ya timu zilichukua ubingwa huu zikiwa pia ni bingwa wa ligi lakini vile vile zipo zilizochukua ubingwa huu bila kuwa bingwa kwenye ligi anapotokea. 
Kwa umri wa miaka 21 ya michuano hii imeshuhudia mabingwa wafuatao:
1. KMKM: 1984
Mwaka huu ulikuwa wa mafanikio kwao kwani licha ya kuchukua ubingwa wa Muungano pia walikuwa ni mabingwa wa ligi ya Zanzibar, hivyo waweza sema walipiga dabo (double) timu hii ilichukua mara moja tu 1984

2. TZ PRISONS: 1999. 
Moja ya nyakati bora za kikosi hiki basi ni mwaka 99 walipochukua kikombr hiki na kukipeleka Mbeya na kujibu mapigo ya Tukuyu stars iliyochukua kombe la ligi 1986. Kama ilivyo kwa KMKM, Tz prisons nao wamechukua mara 1 tu 1999 (Mwaka niliomaliza shule ya msingi )wakati wakichukua kombe hili la Muungano bingwa wa bara alikuwa Mtibwa sugar, hivyo ikawa historia wao kuchukua kombe kwa mara ya kwanza na Mtibwa kutwaa kombe la ligi kwa mara ya kwanza, na kwa mara ya pili makombe yote mawili yanapotea mjini dar es salaam (ya kwanza ni 1986, ligi lilienda mbeya kwa Tukuyu na Muungano likaenda Ruvuma kwa Majimaji) nb:Naruhusu kusahihishwa. 

3. PAMBA SC: 1990
Unawakumbuka hawa mabwana? Historia yao ya miaka ya tisini ni tamu na ya kuvutia sana, Mungu atupe uzima siku moja niandae makala yao peke yao Inshallah. Hawa nao kama KMKM na TZ PRISONS, walichukua mara 1 tu 1990. 

4. MALINDI: 1989 NA 1992. 
Timu hii ni moja ya vilabu vilivyowahi kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF (nitaeleza kwa kina siku nyingine) lakini miaka hii miwili ilikuwa ya neema kwao kwani walibeba vikombe viwili kwa kila mwaka, yaani 1989 walibeba kombe la ligi ya Zanzibar na Muungano, hivyohivyo na mwaka 1992. Moja ya timu tishio sana kwa miaka hiyo soka la Zanzibar lilipokuwa juu kwelikweli. Hawa wamechukua kombe hili mara 2. 

5. PAN AFRICAN. 1982 
Timu tishio iliyotoka kwenye ubavu wa Yanga kutokana na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe, ilikuwa timu tishio haswa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wachezaji waliohama Yanga na kuunda timu hii, historia yake tutapata siku nyingine leo ni Muungano tu ndio naangazia. Wakiwa katika ubora wa hali ya juu walichukua ubingwa wa bara na ule wa Muungano mwaka 1982 na kuweka rekodi ya kumbukumbu kwa kuwa timu ya kwanza kubeba kombe hili mara tu lilipoasisiwa 1982 rekodi ambayo itabaki hivyo kwa muda wote. 

6. AFRICAN SPORTS: 1988. 
Huu ulikuwa ni mwaka wa mkoa wa Tanga, Coastal union wakibeba lile la bara na sports wakibeba la Muungano hivyo makombe yoote kuhamia Tanga wakitoka mikononi mwa Yanga iliyokuwa imeyaweka kabatini kwake. African sports chini mwalimu (Marehemu)Mziray walibeba ndoo hiyo 1988

7.  MAJIMAJI: 1985, 1986 NA 1998. 

Wana bahati na mwaka unapokuwa na namba 8? Sina hakika sana ila ni timu ambayo ukiiandikia makala basi inabidi makl hiyo iwe na sehemu ya pili. (Party 2)kwani tangu kuanzishwa kwake na jitihada za watu wa songea na mfanikio hayo waliyoyapata ni dhahiri kuna mengi ya kuandikwa na kukumbukwa kuhusu ya timu hii. Haijawahi kuchukua makombe mawili kwenye mwaka mmoja kama timu zingine kwani mwaka 1985 wakati wanachukua kwa mara ya kwanza kombe hili la Muungano bingwa wa bara alikuwa YANGA. Mwaka 1986 alipochukua kwa mara ya pili mfululizo kombe la Muungano bingwa wa bara alikuwa Tukuyu stars na mwaka 1998 alipochukua kwa mara ya mwisho bingwa wa bara alikuwa ni YANGA kwa mara nyingine. 

8.  SIMBA SC: 1993, 1994, 1995, 2001 NA 2002. 

Timu pekee kuchukua kombe la Muungano mara 3 mfululizo (sijui kama walipewa kabisa kabisa kama kanuni zilivyokuwa, ndugu yangu Hajji Manara atanikumbusha namba yangu anayo)
Historia iko hivyo na huwezi kuibadili. Tangu kuanzishwa kwa michuano hii 1982 Simba ilihangaika kwa zaidi ya miaka 10 bila mafanikio yoyote mpaka mwaka 1993 (wakiwa na kikosi bora cha muda kwangu mimi nilichokiona kikicheza, sio cha kuhadithiwa)ndipo walipoingia rasmi na kuanza kujimilikisha kombe hili kwa kutwa kwa miaka mitatu mfululizo na kama sio kutokea yaliyotokea basi huenda wangefikia rekodi yao walioweka wenyewe mwaka 2003 (waliokua wanafuatilia wanajua nn kilifanywa na Yanga 2003 chini ya katibu mkuu wake (Namuhifadhi jina kw sababu maalum)hali iliyopelekea michuano hiyo kufa, kama sio hivyo kikosi kile cha 2003 (kilichowatoa Ahly kwenye CCL) basi Simba wangekuwa wametwaa mara 6 kwa staili ya aina yake sababu walibeba 2001 n 2002 kabla ya 2003 michuano hiyo kupotea kabisa. 

Katika mara 5 ambazo Simba imebeba ubingwa huu mara tatu kati hizo walikuwa ni mabingwa wa bara pia, yaani 94, 95 na 2001, kasoro 93 na 2002 ambapo bingwa wa bara alikuwa mtani wake YANGA. 

9. YANGA: 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 NA 2000. 

Katika kombe hili Yanga wana sifa za pekee 3
Moja ni kwamba wao wametwaa kombe la Muungano kuliko vilabu vyote vya Jamhuri ya Muungano (mara 6). 

Sifa ya pili ni kuwa kati ya hizo mara 6 ni mara moja tu yaani mwaka 2000 ndio alikuwa bingwa wa Muungano akiwa sio bingwa wa bara ila mara 5 alikuwa akichukua kotekote. Historia itabaki hivyo na hakuna namna ya kuibadilisha kwamba wao ndio vinara wa michuano hii. 

Sifa ya 3 ambayo sio nzuri kwao ni kwamba wao ndio chanzo cha michuano hii kufa.....  Lakini kama wasemavyo wahenga "Tumbo la shari huzaa kheri" kwa namna moja iliwafungua macho Zanzibar kuomba uanchama CAF ili vilabu vyake vishiriki michuano ya kimataifa. 

Leo hii ni miaka 15 sasa tangu michuano ya ligi ya Muungano ife, michuano ambayo ilifanyika kwa miaka 21 mfululizo. 

Sababu michuano hii ilikuwa inafanyika December nimeona sio vibaya tukakumbushana kidogo. Pale ambako unaona rekodi hazipo sawasawa unaweza kuwasiliana nami *PASCAL KABOMBE* kwa mawasiliano yafuatayo. 

Phone. 0717974030
Email. evarestpascal@gmail.com.
Au wasiliana na mawasiliano ya blog hii kwa namba 0714827331
Email Saidallymwandike@gmail.com
Kama unapenda Kabombe aendelee kushusha makala kwenye blog hii shusha comenti yako hapo chini.
*KHERI YA MWAKA MPYA.

1 comment:

  1. 1992 Bingwa alikuwa Simba tena alishinda kwa Penati dhidi ya Yanga baada ya David Mwakalebela kukosa penati ya Mwisho. Nina mashaka na utunzaji wetu wa kumbukumbu

    ReplyDelete