KAULI YA LIPULI FC JUU YA MCHEZAJI WAO ASANTE KWASSI KUJIUNGA NA SIMBA

Uongozi wa timu ya Lipuli Fc ya mkoani Iringa unapenda kuchukua wasaa huu kukanusha uwepo wa mazungumzo ya aina yoyote na uongozi wa timu ya soka ya Simba SC ya Dar Es Salaam kuhusu kumuuza mchezaji Asante Kwassi kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na vyombo vya habari mbalimbali nchini kwa muda sasa. 

Uongozi unapenda kuwajulisha wanachama, wapenzi na mashabiki wa Lipuli Fc ya kwamba mpaka sasa haujafanya mazungumzo yoyote na timu yoyote kuhusu mchezaji Asante Kwassi na kwa msingi huo uongozi ungependa kukanusha vikali taarifa hizo.

Ikumbukwe mchezaji Asante Kwassi licha ya uwepo wa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii bado ni mchezaji halali wa Lipuli Fc.

Mchezaji Asante Kwassi bado ana si chini ya miezi saba kwenye mkataba wake wa sasa na timu ya Lipuli Fc na kwa muktadha huo bado ni mchezaji halali wa timu ya Lipuli Fc.

Kwa sasa uongozi hauna mpango wowote wa kumuuza mchezaji huo tajwa hapo juu sio tu kwa Simba SC bali pia kwa timu yoyote na kama hapo baadaye kama kutatokea ulazima wa kufanya hivyo uongozi unapenda kutoa ushauri wa bure kwa timu yoyote itakayoonesha matamanio ya kumtaka mchezaji huyo kuwasiliana na uongozi wa Lipuli Fc moja kwa moja ili kuepusha misuguano isiyokuwa na ulazima kwa afya ya familia ya mchezo wa soka nchini.

Mwisho uongozi wa Lipuli Fc unapenda kutoa pole kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wake ambao wamepokea taarifa za kuuzwa kwa mchezaji Asante Kwassi kwa mshtuko mkubwa.

Imetolewa na Afisa Habari Lipuli Fc Clement Sanga.

#WanaPaluhengo

No comments