AZAM YAANZA MCHAKATO WA KUSAKA VIPAJI VYA WANAMICHEZO
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imezidi kutanua wigo kwenye maendeleo ya soka la vijana baada ya kuja na mpango mkubwa wa kutengeneza timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘U-17’.
Ili kuunda kikosi hicho, Azam FC inatarajia kuendesha majaribio kwenye mikoa 13 nchini kwa kipindi cha takribani miezi mitatu, yatakayowahusisha vijana pekee waliozaliwa kuanzia mwaka 2000, 2001 na 2002.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga, Morogoro, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Mtwara, Mbeya na Iringa.
Malengo makubwa ya mradi huo, ni Azam FC kutengeneza kizazi kipya cha vijana baada ya kufanikiwa kupitia mradi wa awali, uliowatoa wachezaji wengi wanaotamba hivi sasa nchini akiwemo winga Farid Mussa, anayetarajia kujiunga na Club Deportivo Tenerife ya Hispania muda wowote kuanzia sasa.
Moja ya masharti kwa vijana wote watakaokuwa wakifanyiwa majaribio kupitia mradi huo mpya, ni lazima wafike na vyeti vyao vya kuzaliwa pamoja na wazazi au walezi wao kwenye siku husika ya majaribio.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz leo kuwa, majaribio hayo yataanza rasmi Jumapili ijayo (Agosti 28, 2016) kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wakianza na vijana wa Wilaya ya Temeke na Kigamboni pekee.
“Kwa siku hiyo watakaopokelewa ni wale pekee wanaotokea Wilaya ya Temeke na Kigamboni, kwa wale ambao watakuwa wanatokea nje ya maeneo hayo, basi kwa terehe hiyo hawataruhusiwa kuja, hivyo tunawaomba wazazi waje na vijana wao wenye vipaji katika maeneo yote tutakayopita nchini,” alisema.
Alisema usajili kwa vijana wote watakaojitokeza utaanza rasmi saa 1.00 asubuhi hadi saa 9.30 jioni, huku asisitiza kuwa suala la umri litazingatiwa kwa vijana wote watakaofanyiwa majaribio hayo.
Ilala je?
Azam FC haijawaacha mbali vijana kutoka Wilaya ya Ilala, kwani mara baada ya zoezi hilo kumamilika Temeke basi litahamia huko, ambapo majaribio yao yatafanyika Septemba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jakaya Kikwete (JMK Park), uliopo Kidongo Chekundu, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kinondoni/Ubungo?
Zoezi hilo litakamilika mkoa wa Dar es Salaam, kwa vijana kutoka Wilaya ya Kinondoni na Ubungo kujaribiwa Septemba 10, mwaka huu katika eneo la Kawe kwenye uwanja ambao tutautangaza hivi karibuni kabla ya siku husika kufika.
Zanzibar kufuatia
Jopo la makocha kutoka timu hiyo, litakalokuwa likiongozwa na Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana la Azam FC, Tom Legg, litahamia Zanzibar na kuendesha majaribio kwa siku mbili Septemba 17 na 18 kwenye Uwanja wa Amaan, Visiwani humo.
Morogoro/Dodoma
Azam FC itaendelea kusaka vipaji katika mikoa mingine, hivi sasa ikihamia mkoa wa Morogoro Oktoba 1 na Dodoma Oktoba 2, katika viwanja ambavyo vitatangaza hapo baadaye.
Arusha/Moshi
Majaribio kwa vijana wa Arusha na Moshi yanatarajia kufanyika Oktoba 8 na 9.
Kigoma/Tabora/Mwanza
Azam FC itahamishia nguvu mkoani Kigoma Oktoba 15 kwa kuendesha majaribio na kuhamia Tabora Oktoba 16, kabla ya kuelekea mkoani Mwanza na kufanya zoezi hilo kwa siku mbili Oktoba 22 na 23.
Mtwara
Mkoa wa Mtwara nao umewekwa kwenye mpango huo wa aina yake, ambapo majaribio hayo yatafanyika kwa siku mbili Oktoba 29 na 30.
Mbeya/Iringa
Timu hiyo inayodhaminiwa na NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, itamaliza zoezi hilo kwa kuwafanyia majaribio vijana wa mkoa wa Mbeya Novemba 5 kabla ya kuhitimisha mkoani Iringa Novemba 6 mwaka huu.
Mchujo mkubwa kufanyika
Kawemba alisema kuwa baada ya zoezi lote la kuzunguka mikoani kukamilika, utafanyika mchujo mkubwa wa kutengeneza kikosi hicho katika majaribio ya mwisho yatakayofanyika Novemba 12 na 13, ambayo yatahusisha vijana wote waliochaguliwa katika mikoa yote iliyohusika.
Alisema kuwa katika mikoa yote waliyozunguka, wataacha wakufunzi watakaokuwa wakiwafundisha vijana wa umri huo ambao watakuwa wamefanya vizuri lakini hawakupata nafasi ya kuchaguliwa.
Alimalizia kwa kusema kuwa mara baada ya kufanikiwa kuunda timu hiyo (U-17), kuanzia mwakani watahamishia nguvu kuunda timu zingine za vijana chini ya umri wa miaka 15 na 12, lengo ni kuiona Azam FC ikivuna wachezaji bora iliyowakuza wenyewe kwa ajili ya kupata mafanikio baadaye.
Moja ya wachezaji walitokana na kituo cha Azam FC Academy na wanaocheza sasa kwenye timu ya wakubwa ni kipa namba moja Aishi Manula, mabeki Ismail Gambo, Gadiel Michael, viungo Mudathir Yahya, Masoud Abdallah, mshambuliaji Shaaban Idd.
Post a Comment