HAJI MANARA AACHIWA HURU

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imefuta adhabu dhidi ya wanafamilia wanne waliofungiwa kushiriki masuala la soka kwa mwaka mmoja.

Wanafamilia hao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa, James Mwakwinya; Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Blassy Kiondo; Kaimu Katibu wake, Ayoub Nyaulingo pamoja na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.

Haji Manara alitiwa hatiani Aprili 23, mwaka huu kwa makosa ya lugha chafu na za chuki kwa viongozi wa TFF na kupotosha umma dhidi ya kadi njano ya mchezaji Mohammed Fakhi wa Kagera Sugar ambako alifungiwa kushiriki masuala ya mpira kwa mwaka mmoja na faini ya Sh milioni tisa.

Viongozi wa RUREFA walifungiwa kwa mwaka mmoja na faini ya Sh. milioni mbili kwa kila mmoja kwa makosa ya kukiuka maagizo ya viongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyotaka wasitishe mchakato wa uchaguzi mkoa kwa kuwa kulikuwa na rufaa iliyokatwa TFF.

Akizungumza na Wanahabari leo Julai 17, 2017 Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Tarimba Abbas, alisema viongozi hao wamesamehewa adhabu zao kwa kuwa waliomba kupitiwa upya kwa mashauri yao na kamati imeona ni bora kuwaachia huru ili kuendeleza masuala ya soka.

“Wapo wengi waliofungiwa wengine maisha na wengine adhabu fupi, msamaha huu ni kwa wale ambao wameomba tu kupitiwa upya kwa adhabu zao, pia milango ipo wazi kwa wengine ambao wanataka kupitiwa kwa mashauri yao, lakini si kwa wale waliopanga matokeo uwanjani,” alisema Tarimba.

Kadhalika, Tarimba aliwaomba viongozi wa TFF kuandaa semina ya Maofisa Habari na Viongozi wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ili kuepuka maneno machafu ambayo yanasababisha wao kufungiwa.

“Inaonekana viongozi na Maofisa Habari hawana maneno mazuri ya kuongea na wadau wa soka na ndio maana matatizo ya kufungiwa yanajitokeza mara kwa mara, naamini wakipata semina hiyo itawasaidia kujirekebisha na kupunguza kesi kama hizo,” alisema Tarimba.

Kwa niaba ya TFF, Ofisa Habari wa Shirikisho, Alfred Lucas, wameyapokea mapendekezo hayo kutoka kwa Tarimba na kwamba tutafanyia kazi ili kurekebisha makosa hayo kwa manufaa ya soka la Tanzania

No comments