WAPO SC YAONYESHA UMWAMBA

Kikosi cha timu ya Wapo SC leo hii kimetoka sare ya 1-1 na timu ya Gospel Team katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa shule ya  sekondar ya Kenton uliyopo maeneo ya Mwenge jijini Dar es salaam.

Katika mechi ya hii leo kikosi cha Wapo SC kilianza kwa kucheza kwa kushambulia zaidi na kufanikiwa kupata bao kunako dakika ya 15 ya mchezo kupitia kwa Kaleb George aliyeachia shuti kali nje ya 18 ambalo lilimshinda mlinda mlango wa Gospel Team John Daniel.


Baada ya goli hilo,timu zote zilianza kucheza kwa kushambuliana ambapo Gospel timu walionyesha uchu wa kusawazisha bao hilo lililofungwa mapema katika kipindi cha kwanza, lakini juhudi hizo hazikuweza kuleta mabadiliko kwa timu hizo kwani hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Wapo SC waliendelea kuongoza kwa bao 1-0.

Katika kipindi cha pili timu zote zilirejea na nguvu mpya ya kiuchezaji huku Gospel Team wakifanya mabadiliko  kadhaa ya wachezaji ikiwemo kwenye nafasi ya  mlinda mlango ambapo John Daniel alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Silas Mbise huku kikosi cha Wapo FC kikishindwa kufanya mabadiliko kutokana na kukosa mchezaji wa akiba lakini haikuwa sababu ya kushindwa kucheza vizuri.



Mabadiliko hayo yaliisaidia zaidi Gospel Team kwani kunako dakika ya 32 walifanikiwa kusawazisha goli lililofungwa na mshambuliaji wa timu hiyo Lucas Mwarabu.

Hata hivyo licha ya kusawazisha bao hilo lakini kikosi cha Wapo Sc kilionekana kucheza kandanda safi na lenye ushindani huku winga wa timu hiyo Barikiel Gadiel ambae pia ndie  meneja wa Wapo Media akionekana kuwa nyota wa mchezo kutokana na kasi yake ya uchezaji akipiga mashuti ya mara kwa mara langoni, yaliokolewa na mlinda mlango Silas Mbise aliyeisadia vyema timu hiyo kutokana na umahiri wake langoni.


Hadi dakika 90 za mchezo timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.


Mara baada ya mechi kuisha viongozi wa Wapo SC,Victoria Mungule, David Gile pamoja na Said Ally Mwandike walitoa lawama kwa mlinda mlango wa Gospel Team Silas ambae walidai kuwa aliweza kuisaliti timu, kwani yeye ni miongoni mwa watangazaji wa Wapo Radio lakini ameshindwa kuitumikia timu yake na kuamua kuchezea timu pinzani.


Kwa upande wa viongozi wa Gospel Team, wao walisema kwamba wameridhishwa na kiwango cha Wapo SC kwani kilionekana kucheza kwa kujiamini zaidi  tofauti na kikosi chao.


No comments