Kipa wa Italia Gianluigi Buffon atacheza mechi yake ya 1000 leo usiku dhidi ya Albania katika mechi za kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia.
Kwa mujibu wa mtandao wa BBC taarifa hiyo inadai kuwa hiyo itakuwa mechi yake ya 168 akiichezea timu ya taifa ya Italia na kumfanya kuwa mchezaji wa kwanza kuichezea timu ya taifa mara nyingi kuliko mchezaji yeyote yule barani Ulaya.
Atakuwa amewawapiku kipa wa Uhispania Iker Casillas na Vitalijs Astafjevs wa Latvia.
Hata hivyo, Buffon anahitaji mechi nyingine 17 ili kuvunja rekodi ya dunia ya mechi 184 inayoshikiliwa na kiungo wa zamani wa Misri Ahmed Hassan.
"Ni furaha isiyo kifani," alisema nahodha huyo wa Juventus mwenye umri wa miaka 39.
Buffon ameshafungwa magoli 799 katika mechi 999 alizochezea klabu yake na timu yake ya taifa.
Alianza kuwa mchezaji wa kulipwa akiichezea timu ya Parma mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 17 na kuitwa katika timu ya taifa miaka 2 baadaye.
Ameshachezea Juventus mechi 612 tangu alipohamia katika klabu hiyo mwaka 2001 Buffon alishinda Kombe la Dunia mwaka 2006.
Awali alisema anapanga kustaafu kucheza soka baada ya michuano ijayo ya Kombe la Dunia nchini Urusi.
Na kwa kutania akaongeza kwamba anapanga kumaliza kama Zinedine Zidane alivyofanya akiichezea Ufaransa katika fainali ya mwaka 2006 kwa kupewa kadi nyekundu.
"Inawezekana nitafanya kama Zidane na kumpiga mtu kichwa uwanjani'' alisema.
Post a Comment