AZAM FC YAREJEA,SABA WAJIUNGA NA KAMBI YA STARS

Kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimerejea jijini Dar es Salaam kikitokea nchini Swaziland kilipoenda kucheza mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows na kufungwa mabao 3-0 juzi.


Azam FC iliyotolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-1, ilianzia safari yake saa 6.15 mchana jijini Johannesburg kwa usafiri wa Ndege ya Shirika la Kenya (KQ) ikipitia nchini Kenya kabla ya kuunganisha ndege iliyowafikisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl Julius Nyerere (JNIA) ilipotua jana saa 3.00 usiku.


Mara baada ya kuwasili wachezaji wa timu hiyo wamepewa mapumziko ya siku mbili hadi Alhamisi ijayo itakapoanza tena mazoezi saa 10.00 jioni kujiandaa na mechi zinazokuja za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).


Wachezaji saba wa Azam FC waliochaguliwa kwenye kikosi kipya cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ nao wamepewa ruhusu ya kujiunga na kambi ya timu hiyo leo Jumanne.


Wachezaji hao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, viungo Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Frank Domayo ‘Chumvi’. 

No comments