KOCHA TP MAZEMBE AFUTWA KAZI

Klabu ya soka ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,imemtupia vilago  kocha wake Thierry Froger.


Hatua hii inakuja chini ya miezi miwili baada ya kupewa kibarua cha kuifunza klabu hiyo aliyekuwa anaichezea mtanzania Mbwana Samata kabla ya kutimkia klabu ya Genk.


Uongozi wa klabu hiyo umesema baada ya matokeo mabaya katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika msimu huu, wameelewana na raia huyo wa Ufaransa kusitisha mkataba wake.


Mazembe ambao ni mabingwa mara tano wa taji hilo, waliondolewa katika michuano ya mwaka huu na CAPS United ya Zimbabwe kwa faida ya bao la ugenini baada ya mchuano wa marudiano kutoka sare ya 0-0 baada ya sare nyingine ya 1-1 katika mchuano wa kwanza mjini Lubumbashi.


Thierry, mwenye umri wa miaka 53 alichukua nafasi ya Mfaransa mwenzake Hubert Velud ambaye alijiuzulu baada ya kuisaidia TP Mazembe kunyakua taji la Shirikisho barani Afrika mwaka 2016.


Baada ya kuondolewa katika michuano ya klabu bingwa, Mazembe sasa itaendelea kushiriki katika michuano ya kuwania taji la Shirikisho ambalo wao ndio mabingwa watetezi.


katika ratiba iliyotolewa na CAF hapo jana klabu hiyo imepangwa kucheza na JS Kabylie ya Algeria katika hatua ya mwondoano, mechi zitakazopigwa mwezi Aprili na mshindi kufuzu katika hatua ya makundi.


TP Mazembe ni msimu wa pili wameshindwa kufanikiwa kufuzu katatika hatua ya makundi katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika ambapo mwaka jana walitolewa kwenye michuano hiyo na kurejea kwenye kombe la shirikisho na kufanikiwa kuwa mabingwa wa kombe hilo.


No comments