KENYA YAFANYA VYEMA KWENYE RIADHA

Wanariadha wa Kenya wametamba katika makala ya 42 ya mashindano ya riadha ya Nyika ya dunia yaliyomalizika Jumapili jioni katika uwanja wa Uhuru wa Kololo jijini Kampala nchini Uganda.


Geoffrey Kamworor alitetea taji aliloshinda mwaka 2015 nchini China baada ya kumaliza mbio za Kilomita 10 kwa upande wa wanaume kwa muda wa dakika 28 na sekunde 24.


Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na mtandao wa RFI nafasi ya pili ilimwendea Leonard Kiplimo Barsoton pia kutoka Kenya, huku Abadi Hadis kutoka Ethiopia akimaliza wa tatu na kushinda medali ya shaba.


Kuelekea kumalizia mbio hizi, Mganda Joshua Kiprui Cheptegei alionekana katika nafasi nzuri ya kumaliza ya kwanza lakini akapatwa na msuli na kupitwa na wanariadha wengine.


Kupitwa kwake kumekuwa pigo kubwa kwa bingwa huyu wa dunia mbio za Mita 10,000 mwaka 2014 kwa wanariadha chipukizi aliyekuwa anashangiliwa na maelfu ya raia wa Uganda.
Cheptegei alimaliza mbio hizo katika nafasi ya 30.


Onesphore Nzikwinkunda kutoka Burundi alimaliza katika nafasi ya 14, huku Mtanzania Gabriel Gerald Geay akimaliza katika nafasi ya 22.


Kenya pia ilifanya vizuri kwa upande wa wanawake baada ya wanariadha wake kumaliza katika nafasi ya kwanza hadi ya sita.


Irene Chepet Cheptai alishinda mbio hizo za Kilomita 10 kwa muda wa dakika 31 na sekunde 57 na kunyakua medali ya dhahabu.


Nafasi ya pili ilimwendea Alice Aprot Nawowuna huku Lilian Kasait Rengeruk akimaliza katika nafasi ya tatu.


Hyving Kipeng Jepkemoi alikuwa wa nne, Agnes Jebet Tirop bingwa mwaka 2015 akimaliza wa tano huku Faith Chepngetich Kipyegon akimaliza wa sita.

No comments