UPEPELEZI WA KESI YA VIONGOZI WA SIMBA WAKAMILIKA

Na Unique Maringo
UPELELEZI wa awali wa kesi ya utakatishaji fesha na kugushi inayomkabili Rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu' umekamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa serikali, Nassoro Katuga alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa upelelezi wa awali wa kesi hiyo umekamilika.

Pia alisema jalada la kesi limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili alisome na kueleza kama anaona umekamilika au lah.

Wakili wa utetezi Philemon Mtakyamirwa alidai kuwa kesi hiyo imefikia katika hatua nzuri.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Nongwa alisema anasubiri maelezo kutoka kwa DPP, ambapo aliahirisha kesi hiyo hadi September 27/2017.

Evans Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za kimarekani 300,000.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  Dola za kimarekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016 Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za kimarekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha,Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa  Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidiaAveva  kujipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

No comments