KOCHA AZAM FC AZITAKA POINTI TATU ZA MWADUI FC
KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, amesema kuwa kikosi chake kimewasili mkoani Shinyanga kwa lengo moja tu la kushinda mchezo dhidi ya Mwadui na kuzoa pointi zote tatu Jumamosi hii.
Kikosi cha Azam FC kimewasili salama mkoani humo siku ya jana kikitokea mkoani Dodoma kilipopata mapumziko ya muda mfupi, ambapo kwa mujibu wa programu ya kocha huyo wachezaji wataanza mazoezi ya kwanza Shinyanga leo jioni kujiandaa na mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Cioaba alisema kuwa kikosi chake kimetua mkoani Shinyanga kikiwa na morali kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo.
“Wachezaji wote wapo tayari hakuna mchezaji majeruhi na morali ipo juu, wote tunaamini kama tutafanya kazi kama familia huku tukiweka tahadhali kwa wapinzani wetu, huwa nawaambia kuwa timu zote zinacheza mpira mzuri haijalishi ni Yanga ama timu yoyote, cha msingi ni kumuheshimu mpinzani na mchezo wenyewe, ninachohitaji ni ushindi siku ya Jumamosi na kupata pointi tatu,” alisema.
Mchezaji pekee ambaye ameshindwa kusafiri na kikosi hicho ni kiungo mkabaji Stephan Kingue, ambaye bado hajapona vizuri majeraha ya mgongo huku winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Shaaban Idd, wakiendelea na matibabu baada ya wote kufanyiwa upasuaji hivi karibuni nchini Afrika Kusini.
Post a Comment