RAIS KARIA APONGEZA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI

Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli leo Jumatatu Oktoba 9, 2017 akiliapisha Baraza jipya la mawaziri, - Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametuma salamu za pongezi kwa mawaziri wote wapya.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli alifanya tena mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi ya Wizara, kuteua Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya na kuwahamisha Wizara baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri.

Taarifa ya Kurugenzi ya Ikulu iliyosainiwa na Gerson Msigwa, ilisema kwamba Mhe. Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alitangaza Baraza hilo  Ikulu jijini Dar es Salaam.


Katika mabadiliko Mhe. Rais Dk. Magufuli ameongeza idadi ya Wizara na Mawaziri wake kutoka 19 hadi 21, na Naibu Mawaziri kutoka 16 hadi 21 na hapo ndipo akamteua tena Mhe. Dk. Harrison George Mwakyembe kuendelea kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Juliana Daniel Shonza kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kutokana na uteuzi huo, Rais wa TFF Karia amewapongeza Waziri Dk. Mwakyembe na Naibu wake, Shonza akisema: “Hongera sana viongozi wetu wapya wa wizara.”

“Lakini pia nipongeze Baraza zima la Mawaziri. Tuna imani na viongozi wetu. Tunaomba mwenyezi Mungu awasaidie mawaziri wote katika kazi zao hasa ikizingatiwa kwamba tuna majukumu mazito katika mpira wa miguu katika mashindano ya kimataifa kwa mwaka ujao.

“Lakini kubwa zaidi, Tanzania tunaandaa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 (AFCON-U17), sasa basi kwa kushirikiana na viongozi wetu wa wizara, tunaamini tutaweza. Tutafanikiwa,” amesema Rais Karia.

No comments