BARAZA LA WADHAMINI SIMBA LAKATAA MKUTANO MKUU
Baraza la wadhamini wa klabu ya Simba linaloongozwa na Khamis Kilomoni limesema kwamba hautambui mkutano mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Akiongea mbele ya waandishi wa Habari leo hii,katibu wa baraza la wadhamini hao Fikilini Mkwabi alisema kwamba wao hawautambui mkutano huo kwani viongozi ambao wameandaa mkutano hawana mamlaka ya kuchukua jukumu hilo la kuitisha mkutano mkuu.
Alisema kwamba kipindi hiki si kipindi cha kujadili hoja ya mabadiliko wakati viongozi wakuu wa klabu waliochaguliwa na wanachama wanatuhumiwa na vyombo vya sheria.
Nao baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ya Simba kwa upande wao wameungana na baraza hilo la wadhamini kwa kutoutambua mkutano mkuu kutokana na viongozi waliopo madarakani kudai hawapo kihalali.
Mmoja wa wanachama hao aliyejitambulisha kwa jina la Said Bedui ameiambia MWANDIKE.BLOGSPOT kwamba kwa upande wao wamebaini kuwa mkutano huo una lengo la kufanya mabadiliko ya katiba ili klabu hiyo iwe katika mfumo wa hisa ambapo kwao jambo hilo hawalitaki kwa kuwa wanachama hawana elimu ya kutosha juu ya mfumo huo.
Post a Comment