KUFUNGA KWAO MBELE YA LIPULI KWA WAPA HAMASA

MABAO ya kwanza yaliyofungwa na washambuliaji wapya wa timu hiyo, Wazir Junior na kinda Yahya Zayd, yamezidi kuwapa matumaini ya kuzifumania nyavu zaidi msimu ujao.
Nyota hao wawili walifunga mabao hayo wakati Azam FC ikiilaza Lipuli ya Iringa mabao 4-0 Jumatano iliyopita kwenye mchezo wa maandalizi ya msimu ujao, mengine yakifungwa na beki Yakubu Mohammed na kiungo Salum Abubakar 'Sure Boy'.
Wakati Junior akisajiliwa na Azam FC akitokea Toto African alikofunga jumla ya mabao saba msimu uliopita, Zayd kwa upande wake amepandishwa kutoka timu ya vijana ya Azam FC ‘Azam FC U-20’.
Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Junior alisema mabeki wajiandae msimu ujao kwani kasi aliyoanza nayo hatairudisha nyuma.
“Bao nililofunga linamenifanya nijisikie vizuri, mchezaji unapokuwa umesajiliwa na timu mpya inachukua muda kuweza kuelewana na wenzako namshukuru Mungu kocha ameendelea kuniamini.
“Bao hili ndio ufunguzi wa ligi, kwa hiyo mabeki wajiandae tu kwa sababu kasi hii niliyoanza nayo haina kurudi nyuma, nitapambana kadiri niwezavyo kuweza kuisaidia timu yangu ya Azam FC,” alisema.
Mbinu za Cioaba zamvuta
Junior hakusita kueleza namna anavyovutiwa na mbinu za ufundishaji za Kocha Mkuu Aristica Cioaba, akisema kuwa kwa kiasi kikubwa mafundisho yake yamemfanya kubadilika na kuwa mwepesi sana tofauti na alivyokuwa awali.
“Kocha huyu ananitaka nitokee pembeni kuelekea kwenye mashambulizi tofauti na Toto nilikuwa nikisimamishwa kama namba tisa, kwa hiyo mbinu zake nimezipenda.
“Uharaka kutoka upande alioniweka hadi kuingia kwenye eneo la penati, umenifanya kuwa mwepesi sana na kwa sasa nahisi nimebadilika sana na natarajia kuwa vizuri zaidi nikiendelea kupata mafunzo yake zaidi,” alisema Junior.
Zayd afunguka
Wakati Junior akimalizia hayo, kinda Zayd naye ameeleza kuwa bao la kwanza alilofunga kwenye kikosi cha wakubwa litamfanya kuongeza juhudi na jitihada za kila hali ili aendelee kufunga zaidi msimu ujao.
“Kuna muda kichwa huwa kinaniuma nikianza kuangalia upinzani ninaotakiwa kukabiliana nao ili kupata namba kwenye kikosi cha kwanza, ukiangalia natokea ‘academy’ halafu bado mdogo nimekutana na watu wenye uzoefu kikosini.
“Najua nakabiliana na upinzani lakini sitochoka, nitaendelea kuvumilia, nitaendelea kupambana kadiri ya uwezo wangu na ipo siku nitapata namba ile ya kuaminika na nitakuwa ni mmoja ya wachezaji tegemeo wa Azam,” alisema Zayd
Mbali na kuwataka mashabiki wa Azam FC kuendelea kuisapoti kwa ukaribu timu yao, pia ameomba uvumilivu wao na sapoti kwake kwa kipindi chote atakachokuwa akipewa nafasi ya kucheza.
“Ndio kwanza naingia kwenye timu nikiwa kama kijana, nimekutana na changamoto nyingine kubwa ya Ligi Kuu sikuwahi kucheza huko nyuma, wasitarajie nitafanya makubwa kila nikipewa nafasi, mimi bado najifunza naahidi nitafanya kazi na pale nitakaposhindwa basi waendelee kunipa sapoti,” alisema.
Zayd amepandishwa kwenye kikosi cha wakubwa mara baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika academy ya timu hiyo, akiwa mmoja ya washambuliaji tegemeo wa kikosi hicho.
Msimu uliopita alitolewa kwa mkopo Ashanti United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), alipokwenda kufanya makubwa zaidi baada ya kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo kwa mabao tisa aliyofunga.
Straika huyo aliyekuwa akichuana na Shaaban Idd ndani ya academy hiyo, aliyepandishwa timu kubwa msimu uliopita pia aliifungia Ashanti jumla ya mabao matatu katika michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

No comments