SIMBA WAJIBU HOJA YA KLABU YA YANGA

Baada ya uongozi wa klabu ya Yanga kuweka bayana msimamo wao mbele ya waandishi wa Habari juu ya kamati ya saa 72 ya TFF kuhusuiana na swala la mchezaji wa Kagera Sugar anaedaiwa kucheza mechi dhidi ya Simba akiwa na kadi tatu za njano.

Mapema leo hii uongozi wa klabu ya Yanga kupitia kwa mjumbe wa kamati ya utendaji Salum Mkemi ulisema kwamba hawana imani na kamati ya saa 72 ya TFF kutokana na kamati hiyo kuwa na idadi kubwa ya wanachama wa Simba huku wakiwasilisha taarifa zao TAKUKURU ili wafanye uchunguzi kwenye kamati hiyo kwani wamedai kuwa kuna viashiria vya rushwa ndani ya kamati hiyo.

Kufuatia taarifa hiyo nao uongozi wa Simba umetoa taarifa kwa vyombo vya habari kuelezea jambo hilo.

Simba Sports Club
Dar es salaam,Tanzania
11-4-2017.
*_TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI_*

Leo mchana huu kunatembea taarifa iliyotolewa na klabu ya Yanga inayoonyesha kuishinikiza Bodi ya ligi kutokutenda haki juu ya rufani yetu dhidi ya klabu ya Kagera Sugar kwa kumchezesha mchezaji Mohammed Fakih aliyecheza dhidi yetu akiwa na kadi tatu za njano ambalo ni kosa kisheria.

Taarifa hiyo ya Yanga iliomnukuu Mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo Salum Mkemi aliyeoongea mbele ya waandishi huku akiwa na katibu mkuu wa klabu hiyo Charles Boniface Mkwasa iliitaka bodi kutokutoa points kwa Simba eti kwa kuwa hizo points zitawaathiri Yanga kwenye kutetea ubingwa wao ambao kwa sasa upo rehani, pia taarifa hiyo imeonyesha Yanga wanao ushahidi kuwa Fakih ana kadi mbili za njano.

Klabu ya Simba inawaambia viongozi wa Yanga wanayo mambo ya msingi ya kuwashughulisha, ikiwepo kutafuta mishahara ya wachezaji wao iliokwama kwa miezi kadhaa kama inavyoripotiwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari,pia waangalie namna bora ya kuurejeshea hadhi uwanja wake wa mazoezi wa Kaunda ili upate kuchezeka tena na sio ulivyo hivi sasa,ambapo umegeuka kama bwawa la kufugia kambale,,ni kushangazwwa kulikochupa mpaka kufuatilia rufani isiyowahusu,Hii ni rufani ya Simba dhidi ya Kagera sio wao Yanga.

Tunaamini bodi haitafanya maamuzi kwa shinikizo la yoyote yule,na hatutarajii kuona porojo walizozisema leo zitaondoa ukweli uliopo mezani kwao ambao klabu yetu imeuwasilisha.

Mwisho niwaombe washabiki wetu watulie na waiachie bodi ifanye maamuzi yake ambayo tunaamini yatatoa haki kwa anayestahili.

IMETOLEWA NA..
Haji S Manara
Mkuu wa Habari wa Simba Sc
*SIMBA NGUVU MOJA*

No comments