KAPOMBE AREJEA UWANJANI
BAADA ya kuwa nje ya dimba kwa takribani miezi mitatu, beki wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, leo asubuhi ameanza rasmi mazoezi mepesi ya gym.
Kapombe, 23, aliyeichezea Azam FC jumla ya dakika 3188 msimu uliopita, hakufanikiwa kumaliza vema msimu baada ya kuugua ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu).
Beki huyo kisiki mwenye kasi ameanza mazoezi akiwa na furaha kabisa hii inaashiria kuwa yupo fiti kabisa kwa ajili ya kurejea dimbani na kuipigania tena Azam FC msimu ujao, ambapo timu hiyo ina wiki ya pili sasa tokea ianze kujiandaa.
Mtaalamu wa Viungo wa Azam FC, Sergio Perez Soto, ndiye aliyemsimamia programu hiyo aliyoanza nayo, ambapo alimfanyisha mazoezi kadhaa ya kumnyoosha viungo kwa kutumia vifaa mbalimbali vya gym.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi hayo, Daktari wa Azam FC, Dr. Juma Mwimbe, alisema kuwa Kapombe ataendelea na programu hiyo mpaka atakapokuwa fiti.
“Tunamshukuru Mungu ameanza mazoezi yake leo, ataendelea na programu ya gym taratibu taratibu hadi wiki ijayo, kama unavyojua hajacheza muda mrefu hivyo tutaendelea kumwangalia zaidi hadi atakapokuwa fiti na baadaye ndiyo tutafanya uamuzi wa kumruhusu kujiunga na wenzake katika mazoezi ya uwanjani,” alisema.
Azam FC vs Friends Rangers
Wakati Azam FC ikiendelea na programu yake ya maandalizi ya msimu ujao kwa siku ya 12 leo, kesho Jumatano inatarajia kucheza mechi ya pili ya kirafiki dhidi ya Friends Rangers inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 3.00 asubuhi.
Jumapili iliyopita Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, aliiongoza timu hiyo kwenye mchezo wake wa kwanza na kwa kuifunga Ashanti United mabao 2-0.
Katika mazoezi hayo ya leo, Azam FC ilimpokea kwenye majaribio mshambuliaji raia wa Burundi, Fuadi Ndayisenga, aliyetokea Sofapaka ya Kenya alipofunga mabao nane msimu uliopita.
Ndayisenga anaungana na wachezaji wengine watatu waliokuwa kwenye majaribio, beki wa timu ya Taifa ya Niger, Mohamed Chicoto na mshambuliaji kutoka huko Mossi Moussa Issa pamoja na Ibrahima Fofana wa Ivory Coast.
Azam FC itacheza mchezo mwingine wa kirafiki Jumamosi ijayo dhidi ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC) kabla ya Jumatatu ijayo kutimkia Zanzibar kwa ajili ya kambi ya kutafuta utulivu kwa wachezaji wakati wakipokea mazoezi ya kiufundi kabla ya kurejea na kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuvaana na Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 17, mwaka huu.
Post a Comment