MUSONYE AIPONGEZA ZANZIBAR HEROES

Na Said Ally
Katibu wa baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati (CECAFA) Nicholas Musonye amekipongeza kikosi cha timu ya Zanzibar Heroes kwa kuendelea kuonyesha kiwango kizuri katika michuano ya kombe la Challenge inayoendelea nchini Kenya.

Musonye alisema katika mashindano ya mwaka huu yanayofanyika nchini Kenya, Zanzibar Heroes imekuwa ikifanya vizuri katika mechi mbalimbali ambazo wamecheza na kuendelea kuwashangaza wengi kutokana na ubora wa kikosi chao.

Alisema kwamba endapo Zanzibar Heroes wataendeleza ubora wao hadi kwenye wa nusu fainali anaamini wana nafasi kubwa ya kufika fainali na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mikubwa kwa ukanda wa (CECAFA).

Aidha Musonye alisema kwamba mashindano ya msimu huu yamekuwa na ushindani wa hali ya juu kwa timu zote ambapo anaamini mshindi wa michuano hiyo atapatikana kihalali kutokana na kiwango chake uwanjani.

Zanzibar Heroes itajitupa uwanjani hapo kesho katika mchezo wa nusu fainali ya pili dhidi ya Uganda mchezo unaotarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa Moi mjini Kisumu kuanzia mishale ya saa 9 alasiri.

No comments