AZAM FC YAIPA MVUVUMWA KIPIGO CHA PAKA MWIZI
IKICHEZA kwa uelewano mkubwa usiku wa kuamkia leo, kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimeichapa mabao 8-1 Mvuvumwa ya mkoani Kigoma katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo huo ulikuwa ni sehemu ya kuwaweka fiti wachezaji wakati huu wa mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliyosimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea kutimua vumbi nchini Kenya.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na winga machachari aliyekuwa kwenye ubora wake, Enock Atta, mshambuliaji Wazir Junior na winga Idd Kipagwile, ambao kila mmoja alifunga mawili huku mabao mengine mawili yaliyobakia yakiwekwa kimiani na kiungo Salmin Hoza na mshambuliaji chipukizi, Paul Peter.
Benchi la ufundi la Azam FC, pia liliutumia mchezo huo kama sehemu ya kuwapa nafasi wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kutosha ya kucheza kwenye mechi za ligi kama vile mabeki wa pembeni, Hamimu Karim, Swaleh Abdallah, beki wa kati David Mwantika, kiungo Masoud Abdallah, ambao walianza katika kikosi cha kwanza.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea tena na programu yake ya mazoezi leo Alhamisi saa 12.00 jioni na keshokutwa Ijumaa kabla ya Jumamosi hii kucheza mechi nyingine ya kirafiki.
Kikosi cha Azam FC Kilichocheza:
Benedict Haule, Swaleh Abdallah/Daniel Amoah dk 43, Hamimu Karim, David Mwantika, Agrey Moris (C), Salmin Hoza, Frank Domayo/Braison Raphael dk 80, Masoud Abdallah/Idd Kipagwile dk 57, Paul Peter/Wazir Junior dk 71, Enock Atta, Joseph Mahundi/Ramadhan Singano dk 68
Post a Comment