MANARA AIBWATUKIA KAMATI YA TFF JUU YA SHAURI LA KAGERA SUGAR

Wakati kamati ya Sheria,Katiba na Hadhi za Wachezaji ikitaraji kutoa maamuzi muda wowote kuanzia sasa juu ya hatma ya pointi tatu na mabao matatu waliyopewa klabu ya Simba,baada ya klabu ya Kagera Sugar kuwasilisha malalamiko TFF wakipinga maamuzi ya kupokwa pointi tatu na kamati ya saa 72 leo hii uongozi wa Simba umeweka bayana juu ya swala hilo.

Akiongea mbele ya waandishi wa Habari leo hii katika makao makuu ya klabu,Mkuu wa idara ya Habari na mawasiliano wa klabu ya Simba,Haji Manara amesema kwamba hakukuwa na haja ya kamati ya Katiba,Sheria na Hadhi za Wachezaji kuitisha kikao kwa ajili ya kujadili marejeo ya shauri la Kagera Sugar kwa madai kuwa haina uhalali wa kufanya jambo hilo.

Manara alisema kwamba uongozi wa Simba unashangaa kuona mtuhumiwa anaitwa kwenye Review au mwamuzi wa nne ambaye hata haandiki ripoti kutoa ushahidi kwenye kamati jambo ambalo ni kinyume na kanuni na halijawahi kutokea.

"Licha ya kikao kutokuwa na uhalali juu ya swala hilo lakini pia kwenye suala la Review hakupaswi kuitwa mashahidi wapya sasa nashangaa kuona wanahojiwa watu ambao katika maamuzi ya awali hawakuwepo"alisema Manara.

Aidha alisema kwamba anashangaa kuona maswala ya klabu ya Simba ambayo yamewasilishwa kwenye kamati za TFF yanashindwa kupatiwa ufumbuzi tena ya muda mrefu lakini kwenye swala la Kagera Sugar kwa sababu lina maslahi kwa upande wao wameamua kulifanya haraka haraka.

Hata hivyo alisema kwamba msimamo wao kama uongozi ni kuona TFF inafanya uhalali na kuendelea kutenda haki kwa kila klabu na endapo watashindwa kufanya uhalali juu ya Review ya Kagera Sugar wanaamini swala hilo litafika mbali kwani wamechoka kuonewa na TFF iliyo chini ya Raisi Jamali Malinzi.

No comments