MAMBO BADO MAGUMU JUU YA MAAMUZI YA RUFAA YA KAGERA SUGAR

Kamati ya Sheria,Katiba na Hadhi za Wachezaji imeshindwa kutoa maamuzi juu ya swala la malalamiko ya Kagera Sugar ikipinga kupokwa pointi tatu na kamati ya saa 72 ya TFF baada ya kamati hiyo kusema kwamba kuna vielelezo bado vinahitajika kwa ajili ya kupata uthibitisho kamili.

Katibu mkuu wa TFF,Selestine Mwesigwa alisema kwamba kwa sasa kuna mashahidi na nyalaka muhimu ambazo zinahitajika ili kulitambua vizuri swala hilo kabla ya kulitolea maamuzi hapo kesho.

Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake Richard Sinamtwa ilianza kulijadili swala hilo kuanzia mishale ya saa nne asubuhi ambapo walianza kuwaita viongozi wa kamati ya Saa 72.

Baada ya kamati hiyo kuwasilisha vielelezo vyao wakafuatiwa na viongozi wa klabu ya Afrika Lyon wakiongozwa na mmiliki wa klabu hiyo Rahim Kangezi Zamunda pamoja na nahodha wa kikosi chake.

Viongozi hao hawakuhojiwa kwa muda mrefu kama ilivyo kwa viongozi wa Kagera Sugar ambao walitumia zaidi ya dakika 40 kuhojiwa na kamati hiyo.

Kamati pia ilipata fursa ya kumuhoji makamu wa Raisi wa klabu ya Simba,waamuzi wa mchezo huo uliowakutanisha Kagera Sugar pamoja na Afrika Lyoni waliyeongozwa na mwamuzi mwenye beji ya FIFA,Donisia Rukyaa aliyekuwa mwamuzi wa akiba kwenye pambano hilo.

Hata hivyo swala hilo linaonekana kuleta utata kwani ni miongoni mwa mambo ambayo yameteka hisia za mashabiki wa mpira wa miguu hapa nchini hususani wa Simba na Yanga.


No comments