MABOSI WA YANGA NA TFF WAWAREJESHA WACHEZAJI DAR

Jumla ya wachezaji 11 wa Yanga na katibu mkuu wa klabu hiyo wanataraji kurejea hapa nchini siku ya kesho mchana baada viongozi wa Yanga waliopo Dar es salaam pamoja na TFF kufanikisha mpango wa kuwapatia tiketi za ndege kwa ajili ya kurejea hapa nchini.

Wachezaji hao 11 waliachwa na ndege kwa siku ya jana baada ya kuchelewa na ikawalazimu kuendelea kuwepo huko hadi siku ya jumatano ya wiki hii.

Katibu mkuu wa Yanga,Charse Boniphace Mkwasa amesema kwamba awali baada ya kukwama uwanja wa ndege waliamua kulipia hoteli hadi tarehe 20, kwani baada ya kuachwa safari ilipangwa tena kurejea siku hiyo ya jumatano.

Mkwasa alisema kwamba klabu haikushindwa kujigaramia kwa siku hizo kama inavyoelezwa na baadhi ya wadau wa mpira wa miguu.

Yanga inataraji kucheza mchezo wa robo fainali ya kombe la FA siku ya tarehe 22 ya mwezi huu,hivyo kurejea kwa kundi hilo ambalo limesalia litarejesha matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa na hofu juu ya ushiriki wao kwenye mechi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons.

No comments