SITA WAFUZU MAJARIBIO KWA WILAYA YA ILALA
VIJANA sita wenye umri wa chini ya umri wa miaka 17 (U-17), wamefanikiwa kufuzu majaribio yaliyoendeshwa na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kwa wakazi wa Wilaya ya Ilala siku ya jana Jumamosi.
Majaribio hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jakaya Kikwete Youth Park (JMK), Kidongo Chekundu, Dar es Salaam, ni ya pili kufanywa na Azam FC katika programu ya kutengeneza timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17.
Kikosi hicho kinachojengwa kupitia mradi huo utakaohusisha kusaka vipaji kwa mikoa 13 nchini, kitaundwa na wachezaji 18 tu ambao watalelewa ndani ya kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam Academy’, ambamo watapata elimu ya kawaida, ya soka pamoja na malazi.
Zoezi la majaribio kwa wilaya hiyo jana, limehudhuriwa na vijana 448 likiwa ni ongezeko la vijana 25, hii ni kutokana na vijana 423 kujitokeza kwenye lile la kwanza lililofanyika Azam Complex Jumapili iliyopita likihusisha wakazi wa Wilaya ya Temeke na Kigamboni.
Kitu cha kuvutia zaidi kwenye majaribio hayo, walijitokeza baadhi ya watoto wadogo chini ya umri wa miaka 13, ambao nao walipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao huku wengine wakilivutia benchi la ufundi.
Idadi hiyo ya vijana sita inafanya kufikia 11, ambao wamechaguliwa mpaka sasa kwenye mchujo wa awali wengine wakiwa ni wale watano waliopitishwa katika mchujo wa kwanza wiki iliyopita.
Mara baada ya kumalizika kwa majaribio hayo, Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, anayeshirikiana na John Matambala, kung’amua vipaji hivyo, alionyesha kuvutiwa na vipaji vya Wilaya ya Ilala huku akidai kupata wakati mgumu kuchagua wachezaji sita wa mwisho.
“Kumekuwa na mabadiliko makubwa hapa kwa vipaji vingi kujitokeza tofauti na Temeke, lakini siwezi kusema Temeke hakukuwa na vipaji, walikuwa wengi lakini hapa wamejitokeza wengi zaidi, zoezi letu leo limekuwa gumu sana hadi tunakuja kupata vijana sita wa mwisho,” alisema.
Kumalizia Kinondoni
Zoezi la kusaka vipaji vya umri huo kwa mkoa wa Dar es Salaam, linatarajia kumalizika Jumamosi ijayo (Septemba 10, mwaka huu) kwa vijana wa Wilaya ya Kinondoni na Ubungo kujaribiwa ndani ya Uwanja wa Tanganyika Packers, uliopo Kawe.
Kuelekea majaribio hayo ya mwisho kabla ya kuhamia mikoani, Legg amesema kuwa ana matumaini ya makubwa ya kupata vipaji vingine bora zaidi katika eneo hilo huku pia akitarajia vijana wengi zaidi kujitokeza.
Azam FC inawaomba vijana waliochini ya umri wa miaka 17, waliozaliwa mwaka 2000, 2001 au 2002 kujitokeza kwa wingi kuonyesha vipaji vyao wakiwa na nakala ya vyeti vyao vya kuzaliwa pamoja na wazazi au walezi wao siku hiyo kuanzia saa 1.00 asubuhi.
Post a Comment