KOZI YA MAKOCHA WANAWAKE YAFUNGWA

Kozi ya makocha wa Mpira wa Miguu imefungwa leo Septemba 9, 2016 saa 5.00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Hosteli ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine ndiye aliyefunga kozi hiyo ambako pamoja na mambo mengine, alitoa shukrani za pekee kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) akisema: “Tunajivunia kwa upendeleo huu, bila shaka ni kwa sababu hata wanafunzi wanaofanya kozi hii, wanafanya vema.”

Mwesigwa amesema kuendelea kutolewa kwa kozi hiyo ni nafasi ya pekee kwa maendeleo ya soka hasa la wanawake hapa nchini.
Akijibu risala la wahitimu wa kozi hiyo ambayo ililenga kuonyesha changamoto ya vifaa vya kufundishia kama vile mipira, vifaa, koni, jezi na filimbi Katibu Mkuu Mwesigwa anasema pia TFF imebanwa na ushuru wa kukomboa vifaa mbalimbali vya maendeleo ya soka bandarini, lakini akaonyesha imani na Serikali ambayo itasaidia.
“Muundo wa kodi pia ni changamoto kwetu,” amesema Mwesigwa na kuondelea: “Kama vifaa kama hivyo mlivyovaa gharama yake ni kubwa, lakini kama ushuru utaondolewa basi tutaendeleza soka na pengine washiriki wanaweza kuwa wengi zaidi ya ninyi.”
Mwesigwa amesema kwamba huu ni mwanzo mzuri wa kuelekea kuwa na benchi la ufundi la wanawake litakalokuwa na makocha wanawake tupu au pengine kuwa na mchanganyiko hata kwenye timu ya wakubwa.
Awali, Mkufunzi wa kozi hiyo ya FIFA, Andrea Rodebaugh Huimon kutoka Mexico alisifu darasa lake la watu 30 ambalo lilipata vyeti vya FIFA akisema: “Lilikuwa zuri na litafika mbali kwa kuwa walikuwa wasikivu, wanaofuata wakati na kushiriki mazoezi vema. Ujumbe huu naupeleka FIFA.”

No comments