KILIMANJARO QUEENS YAFUATA KOMBE UGANDA

Kocha Mkuu wa timu ya Mpira wa Miguu ya Taifa ya wanawake wa Tanzania Bara, Sebastian Nkoma amesema kwamba anakwenda Uganda kwa lengo moja tu, kurejea nchini Tanzania na taji la Afrika Mashariki katika michuano inayoratibiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) maarufu kama Kombe la CECAFA.
Mara baada ya kambi ya kwenda uwanjani na kurudi majumbani kuanzia Septemba mosi, nyota wa timu hiyo ya wanawake wa Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Queens, iliondoka alfajiri ya leo Septemba 5, 2016 kwenda moja kwa moja Bukoba mkoani Kagera ambako itafanya kazi ya siku nne kuanzia Septemba 10, 2016.
Katikati ya kambi hiyo, Kilimanjaro Queens inatarajiwa kuchza na Burundi ambayo pia itakuwa njiani kwenda jijini Jinja, nchini Uganda. Burundi na Tanzania ambazo ziko makundi tofauti, zitacheza mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Septemba 7, mwaka huu.
Michuano ya CECAFA ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki na Kati itafanyika kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016 jijini Jinja, Uganda.
Kwa mujibu wa CECAFA, Tanzania ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa nchi za Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda,.
Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.
Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza na Uganda. Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.
Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.
Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa safari ya Uganda.

No comments