KENYA YAKUBALI KUWAPIMA WANARIADHA WAKE


Kamati ya Michezo ya Olimpiki nchini Kenya, imekaribisha agizo la Kamati ya Kimataifa IOC kutaka wanariadha wake kupimwa kuelekea michezo ya Olimpiki itakayofanyika nchini Brazil mwezi Agosti.

Siku ya Jumanne, IOC ilisema mifumo nchini Kenya na Urusi kushindwa kubaini na kukabiliana na matumizi ya dawa za kuwaongezea nguvu wanamichezo, inakuwa vigumu kuwaamini wanariadha ikiwa hawatumii dawa hizo au la.

Tayari Shirika la Kimataifa linalopambana na dawa hizo WADA limetangaza kuwa Kenya na Urusi zimekuwa zimeonesha kutotoa ushirikiano katika vita dhidi ya janga hilo, hatua ambayo imesababisha Kenya kupitisha sheria ambayo tayari imewasilishwa kwa uongozi wa Shirika hilo.

Mkuu wa michezo ya Olimpiki nchini Kenya Kipchoge Keino amesema tayari wanariadha zaidi ya 60 wakiwemo wachezaji wa mchezo wa raga tayari wameshafanyiwa uchunguzi huo na mwingine utafanyika kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki.

Miongoni mwa wanariadha ambao tayari wameshafanyiwa uchunguzi huo ni pamoja na wale watakaoshiriki katika mashindano ya duniani ya riadha kwa vijana wasiodizi miaka 20, yatakayofanyika mwezi Julai mjini Bydgoszcz, nchini Poland

Nchi ya Kenya ni moja ya nchi ambayo imekua ikijipatia umaarufu mkubwa katika sekta ya michezo hasa kupitia mchezo wa Riadha ambao hua washiriki kutoka nchi hiyo mara nyingi hua wanafanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

No comments