AKILIMALI ASEMA YEYE HAKATAI MABADILIKO KAMA INAVYOELEZWA

Na Said Ally
Katibu wa baraza la wazee wa klabu ya Yanga,Ibrahim Akilimali amesema kwamba yeye hakukataa mabadiliko ya uendeshaji wa timu kama inavyoelezwa na baadhi ya viongozi wa matawi ya klabu ya Yanga.

Akilimali ameiambia MWANDIKE.BLOGSPOT,kwamba viongozi hao wanaosema yeye anakataa mabadiliko ni waongo na wana nia mbaya ya kutaka kumgombanisha na viongozi wajuu wa klabu na wanachama wa timu hiyo.

"Hilo wananisingizia na wanaona haya,mimi sijapinga maendeleo ndani ya Yanga na nasema kwa dini yangu sitakataa mabadiliko ndani ya Yanga, ni mimi mmoja na wazee wenzangu 30 tuliotembea Tanzania nzima kupelekea Yanga iwe na kampuni yake mwaka 2006,sasa leo hii mimi tena huyo huyo nikatae maendeleo? hao ni waongo"alisema Akilimali.

Alisema kwamba yeye alichokisema ni kuutaka uongozi uanze mchakato wa uchaguzi ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na mwenyekiti wa klabu hiyo aliyejiuzulu.

"Kama uongozi unashindwa kufanya uchaguzi mkuu ili kusubili hatma ya Yusufu Manji basi ni vyema uharakishe mapema kuitisha mkutano mkuu wa wanachama ili kulijadili swala hilo lakini sio kusubiri  kwa muda mrefu hadi huo mwezi wa pili ndio uitishwe mkutano mkuu"

Aidha Akilimali amewaomba wanachama wa klabu hiyo kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki ili kuhakikisha kuwa kikosi chao kinafanya vizuri katika michezo ya ligi kuu Tanzania bara pamoja na michuano ya kimataifa.

Mapema leo hii viongozi wa matawi 63 ya Dar es salaam ya klabu ya Yanga kwa pamoja waliadhimia kuwasilisha ajenda katika kamati ya utendaji ili Ibrahimu Akilimali afutwe uwanachama katika mkutano mkuu kutokana na mwanachama huyo kuushutumu uongozi wa klabu mara kwa mara kupitia vyombo vya habari.

No comments