WANACHAMA YANGA WAAMUA KUMFUTA UWANACHAMA IBRAHIM AKILIMALI
Na Said Ally
Viongozi wa matawi 63 ya Dar es salaam ya klabu ya Yanga,leo hii walikutana makao makuu ya timu hiyo kujadili maswala mbalimbali ikiwemo swala la katibu wa baraza la wazee Ibrahim Akilimali kushutumu taratibu ambazo zinaendelea ndani ya klabu hiyo.
Mwakilishi wa Matawi ya Yanga Robert Kasela alisema kwamba kwa pamoja viongozi hao wa matawi wamekubaliana kwamba swala lake lipelekwe katika mkutano mkuu ili lijadiliwe na wanachama.
Alisema kwamba wao kama viongozi wanalaani vikali tabia za Akilimali kuzungumza kauli ambazo hazina msingi na zenye lengo la kuleta mgogoro katika klabu ya Yanga.
Nae makamu mwenyekiti wa tawi la Yanga la Uhuru Kariakoo Kais Edwin aliongeza kwa kusema kuwa kwa pamoja viongozi hao wa matawi wamekubaliana kupeleka ajenda kwa kamati ya utendaji ili kuomba mzee Akilimali akafutiwe uwanachama wake katika mkutano mkuu.
Aidha alisema kwamba hii si mara ya kwanza kwa Akilimali kuushutumu uongozi, hivyo kama uongozi utaendelea kumfumbia macho anaamini ataendelea kuleta mvurugano kwa viongozi na wanachama wa klabu ya Yanga.
Hata hivyo alisema kwamba kwa upande wao kama wanachama wanaungana na uongozi katika swala la kuibadili klabu kujiendesha katika mfumo wa Hisa kwani kwa nyakati za sasa uendeshaji wa mpira wa miguu unahitaji gharama kubwa.
Post a Comment