WACHEZAJI SITA WA AZAM FC WAITWA NGORONGORO HEROES

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoa wachezaji sita katika kikosi cha awali cha timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes).
Wachezaji hao ni miongoni mwa vijana 50 walioitwa kwenye kikosi hicho na Kocha Mkuu, Kim Poulsen, kitakachojiandaa na michuano ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika nchini Niger mwaka 2019.
Wachezaji wa Azam U-20 walioitwa ni beki wa kati Oscar Masai, kiraka anayecheza nafasi zote za ulinzi pembeni na kiungo cha ukabaji, Ramadhan Mohamed ‘Ramaninho’, beki wa kushoto Said Issa, viungo Rajabu Odasi, Mohamed Abdallah 'Kijiko' na mshambuliaji Paul Peter aliyeongezwa leo Jumatatu.
Peter ameongezwa kwenye kikosi hicho baada ya kuonyesha kiwango cha juu wikiendi iliyopita alipokuwa na kikosi cha Azam FC baada ya kufunga bao la kusawazisha lililoipa pointi moja timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Singida United ulioisha kwa sare ya bao 1-1.
Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa nchini ya NMB na Tradegents, imekuwa na programu endelevu za timu za vijana kwenye kituo chake kukuza vipaji cha Azam Academy, ambacho kimekuwa na msaada mkubwa wa kuijenga timu hiyo na kulinufaisha Taifa kwa ujumla.
Wawili Taifa Stars kuripoti
Wakati huo huo, wachezaji wawili wa timu kubwa nahodha Himid Mao ‘Ninja’ na mshambuliaji Mbaraka Yusuph, walioitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wanatarajia kuripoti kambini leo mara baada ya Azam FC kurejea jana jijini Dar es Salaam kilipokwenda kucheza na Singida United mkoani Dodoma.
Stars inaingia kambini kujiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki ulioko kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) dhidi ya Malawi unaotarajia kufanyika Jumamosi hii.

No comments