DOMAYO AELEZA SABAU ZA AZAM KUSHIKAMANA

Kiungo nyota wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Frank Domayo ‘Chumvi’, amesema kuwa moja ya vitu vinavyowabeba hadi kufanya vizuri ni timu hiyo kucheza kwa pamoja na kushikamana kama timu.
Tokea msimu huu uanze, Azam FC imekuwa na mwenendo mzuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) hadi sasa timu zote zikiwa zimeshacheza mechi tano kila moja, mabingwa hao wamejikusanyia jumla ya pointi 11 katika nafasi ya tatu sawa na Mtibwa Sugar na Simba zilizo juu yake kwa tofauti ya mabao ya kufunga.
Domayo amesema kuwa wamekuwa na ushirikiano, kuonyeshana upendo na kusaidiana kwa kila jambo nje na ndani ya uwanja.
“Siri ya mafanikio ni kujituma, kufanya mazoezi kuishi na watu pamoja wachezaji wenzangu tunaoshirikiana uwanjani, kupendana, mkipendana siku zote mnasaidiana kwa kila jambo kama mtu umekosea tunakupa moyo, sehemu mtu ya kufunga unamwekea mwenzako, kwa hiyo naweza kusema tunacheza kwa pamoja ili tuweze kufanya vizuri,” alisema.
Kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha timu mbele na kusaidia ukabaji, amesema kuwa wanapambana ili waweze kushinda kila mechi wanayoingia dimbani ili timu hiyo iwe na mwisho mzuri.
“Kwa hiyo tunapambana kadiri ya uwezo wetu kila mechi inayokuja ili tuweze kufanya vizuri na tuweze kushinda, kila timu ina changamoto, kwa hiyo kama hamna changamoto kunakuwa hamna kitu kwenye timu, naweza kusema kuwa tunapambana kila mtu kwenye nafasi yake, unapigania namba yako ili uweze kucheza vizuri kila mechi ili uweze kudumu kwenye kikosi.
“Kuna wachezaji wengi wazuri kocha mwenyewe anachagua kwa hiyo unapambana kwenye nafasi yako, unafuata maelekezo ya kocha na unacheza kulingana na kocha anachokuagiza uwanjani ili uweze kumshawishi aweze kukupa nafasi,” alisema.
Azam FC kurejea mzigoni  
Baada ya mapumziko ya siku mbili jana na leo Jumanne, kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa nchini ya NMB na Tradegents, kinatarajia kurejea tena mazoezini kesho Jumatano jioni kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mwadui unaotarajia kufanyika Uwanja wa Mwadui Complex Oktoba 14 mwaka huu

No comments