AZAM FC KUJIMA NGUVU NA NGORONGORO HEROES

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki wa mazoezi dhidi ya timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ keshokutwa Jumamosi Oktoba 7, utakaofanyika Uwanja wa JMK Park, saa 1.00 asubuhi.
Mchezo huo ni maalumu kabisa kwa ajili ya vikosi hivyo kujiweka sawa na mechi zilizo mbele yao, Ngorongoro ikijiandaa na mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika nchini Niger mwaka 2019.
Azam FC yenyewe inajiwinda na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwadui utakaofanyika Uwanja wa Mwadui Complex Oktoba 14 mwaka huu, pamoja na ule wa mkoani Mwanza watakaochuana na Mbao utakaopigwa Oktoba 21 kwenye Uwanja wa Kirumba.
Kikosi cha Ngorongoro kinaundwa na wachezaji 50, wakiwemo wachezaji sita wa Azam U-20, ambao ni beki wa kati Oscar Masai, mabeki wa pembeni Ramadhan Mohamed ‘Ramaninho’, Said Issa ‘Shilla’, viungo Rajab Odasi ‘Stam’, Mohamed Abdallah ‘Kijiko’ na mshambuliaji Paul Peter ambaye hivi karibuni amepandishwa timu kubwa.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, aliyeanza rasmi programu yake jana jioni kuelekea mechi zijazo la ligi, atautumia mchezo huo kuwasoma wachezaji wake pamoja na kuwaweka kwenye ushindani kutokana na wikiendi hii kutokuwa na mechi yoyote ya ligi kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Katika kalenda hiyo, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Malawi, unaotarajia kufanyika Uwanja wa Uhuru Jumamosi hii saa 10.00 jioni, ambapo wachezaji wawili wa Azam FC, nahodha Himid Mao ‘Ninja’ na mshambuliaji Mbaraka Yusuph, wamechaguliwa kujiunga na kikosi hicho.

No comments