AZAM FC YAICHAKAZA URA
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendelea kufanya kweli kwenye kambi yake nchini Uganda baada ya muda mchache uliopita kuichapa URA mabao 2-0.
Mchezo wa huo wa kimataifa wa kirafiki ulifanyika Uwanja wa Phillip Omondi, ambapo Azam FC imeutumia kama maandalizi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alichezesha kikosi kingine cha pili katika mchezo huo na kuwapumzisha wachezaji walioanza kwenye mechi mbili zilizopita.
Mabao yote mawili ya Azam FC yamefungwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, moja katika kila kipindi cha mchezo huo, la kwanza akifunga dakika ya 19 kwa shuti kali nje ya eneo la 18 kabla ya kutupia jingine la aina hiyo dakika ya 47.
Licha ya mabadiliko makubwa kikosini kwenye mchezo huo, bado timu hiyo ilionekana kucheza na kuwa imara kwenye eneo la ulinzi huku kipa Mwadini Ally, akifanya kazi kubwa baada ya kuokoa michomo mingi ya URA.
Mara baada ya mchezo huo wa tatu wa kirafiki kwenye kambi ya timu hiyo nchini Uganda ambapo jana ikitoka sare ya bao 1-1 na mabingwa wa Uganda KCCA, Azam FC itashuka tena dimbani Jumapili ijayo kumenyana na Onduparaka, mtanange utakaofanyika Uwanja wa Nambole kuanzia saa 10.00 jioni.
Ziara hiyo itahitimishwa Jumatatu ijayo kwa Azam FC kucheza mchezo wa tano wa kirafiki dhidi ya washindi wa tatu wa Ligi Kuu Uganda msimu uliopita, Vipers FC, utakaofanyika Uwanja wa St Marys uliopo Kitende, Uganda.
Kikosi cha Azam FC leo:
Mwadini Ally, Swaleh Abdallah, Hamimu Karim, Abdallah Kheri, David Mwantika (C), Stephan Kingue, Idd Kipagwile/Braison Raphael dk 57, Salmin Hoza/Frank Domayo dk 84, Yahaya Mohammed/Yahya Zayd dk 70, Enock Atta/Masoud Abdallah dk 55, Joseph Mahundi/Ramadhan Singano dk 81
Post a Comment