LICHA YA KUFUNGWA AZAM FC YAWAFURAHISHA MASHABIKI

Licha ya kupoteza kwa mabao 4-2 dhidi ya Rayon Sports, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kuwafurahisha mashabiki wa soka nchini Rwanda kutokana na kiwango kizuri ilichokionyesha jana jioni katika Uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali.
Azam FC ambayo ndio kwanza imeanza maandalizi ya msimu ujao kwa kufanya mazoezi takribani siku nane, ilisheheni kikosi chenye wachezaji wengi wapya katika kila idara lakini iliweza kuwaonyesha ushindani wa kweli mabingwa hao wa Rwanda.
Rayon Sports iliweza kuutumia mchezo huo kukabidhiwa kombe lao la Ligi Kuu ya Rwanda (Azam Rwanda Premier League) mbele ya mashabiki wao na Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA).
Wenyeji hao ndio walikuwa wa kwanza kuandika bao, likifungwa dakika ya 30 na Pierre Kwizera kabla ya dakika 11 baadaye Mudathir Yahya kuisawazishia Azam FC kwa bao la kiufundi akitumia vema pasi safi aliyopewa na Yahaya Mohammed.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, timu hizo ziliweza kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa sare hiyo.
Azam FC iliongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji kwa kukianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko, akitoka Idd Kipagwile aliyeumia na kuingia Joseph Mahundi.
Savio Nshuti, aliendelea kuwaweka mbele wenyeji kwa kufunga bao la pili dakika ya 49 baada ya kutokea uzembe kwenye safu ya ulinzi ya Azam FC.
Alikuwa ni Yahaya aliyekuwa kwenye kiwango kizuri, ambaye aliisawazishia Azam FC dakika ya 55 baada ya kupenyezewa pasi safi ya kichwa na Yahya Zayd kabla ya kuwazidi maarifa mabeki wawili na kuingia ndani ya eneo la 18 kisha kupiga mpira uliomshinda kipa wa Rayon, Eric Ndayishimiye.
Kuelekea dakika 23 za mwisho za mchezo huo, Rayon Sports waliweza kujipatia mabao mawili yaliyowapa ushindi, kupitia kwa Kevin Muhire dakika ya 67 na Shassie Nahimana dakika ya 90.
Dakika ya 90 almanusura Azam FC iandike bao la kusawazisha baada ya Kimwaga kumhadaa Niyonzima na kuingia ndani ya eneo 18 pembeni kutoka eneo la kupiga kona, lakini pasi yake safi inakosa mmaliziaji.
Kufuatia kushiriki kwenye mchezo huo maalumu wa kusheherekea ubingwa wa Rayon, Azam FC iliweza kukabidhiwa tuzo maalumu na wenyeji wao hao kwa kushirikiana na FERWAFA.
Mara baada ya mtanange huo, kikosi cha Azam FC kimeshaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam leo alfajiri na kinatarajia kupata mapumziko mafupi mkoani Dodoma kabla ya kesho Jumatatu kuwasili jijini humo kuendelea na maandalizi ya msimu mpya chini ya Mromania Aristica Cioaba, ambaye ameshawasili.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:
Mwadini Ally/Metacha Mnata dk 75, Ismail Gambo/Ramadhan Mohammed dk 75, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri/Stanslaus Ladislaus dk 70, David Mwantika (C), Frank Domayo, Masoud Abdallah, Mudathir Yahya/Abbas Kapombe dk 58, Yahaya Mohammed/Joseph Kimwaga dk 58, Yahya Zayd, Idd Kipagwile

No comments