TP MAZEMBE YAFUZU KWA KISHINDO MICHUANO YA SHIRIKISHO

Timu ya TP Mazembe imefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika kwa kishindo baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi kwa kuifunga timu ya Horoya FC kwa jumla ya magoli 2-1.

Kufuatia ushindi huo wa magoli 2-1 TP Mazembe imekamilisha mechi hizo za hatua ya makundi kwa kuongoza kundi D kwa alama 12 akifuatiwa na timu ya SuperSport United katika nafasi ya pili kwa alama 10 nao pia walishinda mechi ya mwisho kwa magoli 4-1 dhidi ya CF Mounana ambao moja kwa moja timu hizi zinasonga katika hatua ya robo fainali.

Timu nyingine ambazo hapo jana zilikata tiketi ya kucheza robo fainali ni pamoja na CS Sfaxien na MC Alger katika kundi B.

Mechi nyingine ya michuano hiyo inaendelea leo hii katika kundi C, ambapo timu ya Recreativo do Libolo watakwaana na Smouh SC.

Zesco United ya Zambia tayari imefuzu kutoka kundi C, baada ya mchuano wake dhidi ya Al-Hilal ya Sudan kuondolewa katika michuano hii.

Klabu ya KCCA ya Uganda, iliteleza katika mchuano wake wa mwisho siku ya Ijumaa dhidi ya Club Africain Tunisia baada ya kufungwa mabao 4-0 katika mchuano wa  kundi A.
Matokeo haya, yameifanya KCCA kukosa nafasi ya kuingia katika hatua ya robo fainali licha ya kuanza vizuri michuano hii  kwa kushinda mechi 3 na kwa bahati mbaya kupoteza mechi tatu.
KCCA inayofunzwa na kocha Mike Mutebi imelazimika kuaga mashindano haya kwa alama 9 ikiwa katika nafasi ya tatu, huku FUS Rabat ya Morroco ikifanikiwa kufuzu ikiwa na alama tisa kwa sababu ina mabao 9 huku KCCA ikiwa na mabao 8.
Mbali na FUS Rabat, Club Africain imefuzu baada ya kumaliza ya kwanza kwa alama 12.

No comments