MWAKYEMBE ATOA SIKU MBILI MUAFAKA UPATIKANE

Waziri wa habari Utamaduni Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Dk Harison Mwakyembe ametoa siku mbili mgogoro baina ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kushughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi ili uishe moja kwa moja.
Dk Mwakyembe aliagiza hayo jana nyumbani kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Oysterbay, Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys wanaokwenda Morocco kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na fainali za Afrika nchini Gabon mwezo ujao.
Mwakyembe amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake akutane na Katibu wa Wizara ya Fedha na kwa pamoja wakakae na Kamishna Jenerali wa TRA ndani ya siku mbili wazungumze na kutatua tatizo hilo.
"Ikishindikana hiki kikao kufanyika (Mama Samia) nitakuja kushitaki kwako. Hicho kikao naomba kifanyike kama nilivyoagiza mapema, sitaki kusikia tena kuhusu hilo deni,"alisema Dk Mweakyembe na kuongeza;."Ninaogopa nisipoyasema haya mapema (TRA), watakuja kukamata basi wakati linakwenda Uwanja wa Ndege tukachelewa ndege ya kwenda Morocco,".
Dk. Mwakyembe alisema anachukua hatua hiyo kwa sababu baada ya kulifuatilia deni lenyewe linaoikabili TFF linaonekana ni la Serikali. Kauli ya Dk Mwakyembe ilifuatia TRA kupitia kampuni ya udalali na minada ya Yono kukamata basi la timu ya taifa, Taifa Stars ambalo kwa sasa linatumiwa na timu ya Serengeti Boys.
Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema kwamba basi lilichukuliwa katika hoteli ya Urbun Rose, Kisutu, Dar es Salaam likiwa linawasubiri wachezaji wa Serengeti Boys liwapeleke kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu.
Hatua hii inakuja kiasi cha wiki tatu baada ya TRA kupitia Yono pia kuzifunga ofisi za TFF kutokana na deni kubwa la kodi na la muda mrefu.Deni hilo la Sh. Bilioni 1.2 linatokana na kodi za mishahara ya waliokuwa makocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo na Mdenmark, Jan Borge Poulsen kuanzia mwaka 2010 hadi 2016.
Tayari TFF chini ya Rais wake, Jamal Malinzi imefanikiwa kulipa deni lingine la zaidi ya Sh. Milioni 400 kodi ya Ongezeko la Thamani (VaT) la ziara ya timu ya taifa ya Brazil nchini mwaka 2010 ilipokuwa njiani kwenye Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Hata hivyo tayari basi ambalo liliwabeba wachezaji wa timu ya Serengeti boys limeachiwa huru ili liendelee kuwasaidia vijana hao kwenye mizunguko yao.

No comments