KOCHA AZAM FC ATAMBA KUIFUNGA YANGA JUMATANO
KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa ana uhakika mkubwa wa kuifunga Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumatano ijayo.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, itaivaa Yanga katika mchezo huo utakaofungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) 2016/2017 utakaoanza Agosti 20 mwaka huu.
Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya URA ya Uganda (1-1) uliofanyika jana usiku, Zeben alisema ameweka mkazo kwenye mechi hiyo na anaamini ya kuwa ataifunga timu hiyo kutokana na jitihada anazofanya kukijenga kikosi chake.
“Siwezi kuzungumzia sana mechi ya Yanga kwa sababu kwani naamini ya kuwa jitihada zangu na taalamu ninayowapa wachezaji wangu naamini itatoa matunda, lakini natambua ya kuwa Yanga ni timu ya zamani ipo na inacheza vizuri, kikubwa naamini nitashinda mchezo huo kulingana na kile ninachowapa wachezaji wangu,” alisema.
Akizungumzia mchezo wa mwisho wa kirafiki waliocheza na URA, Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kikosi chake kimecheza vema na kudai kuwa tatizo kubwa lipo kwenye kumaliza mchezo kwa kufunga mabao.
“Naamini kwa kuwa bado naendelea kuwanoa wachezaji wangu, naamini hali itabadilika na mabao yatakuwa yakipatikana kama kawaida…Lakini kwa sasa pia kuna upungufu pia kwenye nafasi ya mabeki wa kati baada ya kuumia kwa Aggrey (Morris), Wawa (Pascal), kwa kipindi ambacho wanaendelea na mazoezi mepesi naamini wakirudi tatizo hilo litaondoka pia,” alisema
Mechi nyingine saba za kirafiki za awali za Azam FC, ilizifunga Friends Rangers (2-1), Ashanti United (2-0), Mshikamano (1-0), Kombaini ya Wilaya ya Mjini (1-0), Taifa Jang'ombe (1-0), na sare mbili ilipocheza na JKT Ruvu (1-1) na Ruvu Shooting (1-1).
Baada ya mchezo huo wa Yanga, Azam FC inatarajia kuanza kuwania taji la ligi kwa kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya timu iliyorejea Ligi Kuu African Lyon, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Agosti 20 mwaka huu.
Post a Comment