KENYA YAENDELEA KUTAMBA KATIKA MASHINDANO YA OLIMPIKI
Kenya imeendeleza rekodi yake ya kushinda medali ya dhahabu katika mbio za Mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa upande wa wanaume katika mashindano ya Olimpiki.
Kipruto mwenye umri wa miaka 21, alimaliza mbio hizo kwa muda wa dakika 8, sekunde 3 nukta 28 baada ya kuongoza mbio hizo kutoka mwanzo hadi mwisho na kuweka rekodi mpya ya Michezo ya Olimpiki.
Mwaka 2013 jijini Moscow nchini Urusi na 2015 jijini Beijing nchini China wakati wa mashindano ya dunia ya riadha, Kipruto alimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Kemboi lakini hatimaye ndoto yake ya kunyakua dhahabu imetimia.
Bingwa wa mwaka 2012 na 2004 Ezekiel Kemboi mwenye umri wa miaka 34, alimaliza katika nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 8 sekunde 8 nukta 47, huku wachambuzi wa riadha wakisema kutoka na umri mkubwa ameshindwa kufanya vizuri na sasa anaelekea kustaafu riadha.
Licha ya kumaliza katika nafasi ya tatu, Kemboi ataendelea kuwa katika vitabu vya historia kwa kuwa mwanariadha aliyewahi kushinda mara tatu mfululizo mashindano makubwa ya dunia, mwaka 2011 huko Daegu Korea Kusini, Michezo ya Olimpiki mwaka 2012 jijini London na Mashindano mengine ya riadha ya dunia mwaka 2013 jijini Moscow nchini Urusi.
Kenya haijawahi kushindwa katika mbio hizi tangu mwaka 1968, na hivyo kuwa bingwa wa dunia.
Wanariadha wengine ambao wameishindia Kenya medali ya dhahabu katika mbio hizi ni pamoja na Kipchoge Keino-1972 mjini Munich, Julius Korir-1984 mjini Los Angeles, Julius Kariuki -1988 mjini Seoul, Mathew Birir-1992 mjini Barcelona, Joseph Keter -1996 mjini Atlanta na Reuben Kosgei- 2000 mjini Sydney.
Post a Comment