AZAM VS YANGA NI VITA YA KISASI LEO HII TAIFA



KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo saa 10.30 jioni itakuwa na kibarua kizito pale itakapokuwa ikivaana na Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii unaoshiria kufunguliwa kwa pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) 2016/17.
Kikosi cha Azam FC kinaingia kwenye mchezo huo kikiwa na morali kubwa kutokana na maandalizi mazuri iliyofanya chini ya makocha wapya kutoka Hispania, wakiongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez.
Ukiachilia mbali ujio wa makocha wapya, pia kuna baadhi ya sura kwa upande wa wachezaji, Azam FC ikiwasajili Wazimbabwe Bruce Kangwa, Francisco Zekumbawire, Muivory Coast Gonazo Bi Thomas, Waghana Enock Atta Agyei na beki kisiki Daniel Amoah.

Kwa upande wa timu ya soka ya Yanga wanataraji kuingia katika pambano hilo huku wakiwa bado wapo kwenye ushiriki wa michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika licha ya kushindwa kufuzu kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo lkn kikosi chao kitakua na faida kubwa ya wachezaji wake kuwa pamoja kwa muda mrefu huku kukiwa hakuna mabadiliko kwenye benchi la ufundi kama ilivyo kwa Azam.

Yanga leo hii inakutana na Azam huku wakiwa na wachezaji 5 wapya ambao wamesajiliwa msimu huu akiwemo Obrey Chirwa,Hassani Ramadhani Kessy,Juma Mahadhi,Andrew Dante na Beno Kakolanya.

Rekodi/Takwimu
Hii ni mara ya nne timu hizo kukutana kwa mwaka huu, ambapo Januari walikutana kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi na kuisha kwa sare ya bao 1-1, mtanange huo ulifuatiwa na ule wa mzunguko wa wa pili wa ligi ambao uliisha kwa sare nyingine ya 2-2 kabla ya Yanga kushinda 3-1 katika fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).
Katika hatua nyingine, hii ni mara ya nne mfululizo kwa timu hizo kukutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Yanga ikifanikiwa kuibuka na ushindi mara zote.
Walianza kukutana mwaka 2013, Yanga wakishinda bao 1-0, lililofungwa na Salum Telela, ikashinda tena 3-0 (2014) kabla ya mwaka jana kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 8-7 kufuatia sare ya 0-0 baada ya dakika 90 za muda wa kawaida kumalizika.

No comments