MICHUANO YA KOMBE LA MEI MOSI IRINGA,IKULU YATWAA UBINGWA

Na Mwandishi Wetu
WAKATI timu ya Ikulu ikitetea ubingwa wake wa netiboli kwa kuifunga Uchukuzi katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU), nayo timu ya Geita Gold Mine (GGM) imeambulia nafasi ya tatu katika mchezo wa soka wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Ikulu ambao wanawatumia wachezaji warefu na wepesi wakiongozwa na kocha wao mzoefu Mary Protas waliwafunga Uchukuzi kwa taabu iliyoongozwa na kocha wake mchezaji Judith Ilunda kwa magoli 31-20. Washindi wakimtegemea mfungaji wake Fatuma Machenga aliyefunga magoli 31 walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 17-9.
Magoli ya Uchukuzi yalifungwa na mchezaji mkongwe Matalena Mhagama magoli 13 na Bahati Herman magoli saba. Uchukuzi imetwaa kombe la ushindi wa pili kwa matokeo hayo.
Katika mchezo soka wa kutafuta mshindi wa tatu timu ya GGM iliyovuliwa ubingwa na Tumbaku, sasa imeambulia nafasi ya tatu kwa kuwashinda Uchukuzi kwa mbinde baada ya kupigiana penati 6-5, baada ya kumaliza dakika 90 za kawaida bila kufungana.
Timu hizo zilipigiana penati tisa kila mmoja, lakini GGM walikosa tatu na Uchukuzi walikosa nne, ambapo waliofunga penati za GGM ni Mohamed Salum, Oswald Binamungu, Yusufu Paul, Amos Mrutu, Enock Magole na kipa  Emmanuel Sangra, huku waliokosa kwa kupaisha na nyingine kudakwa na kipa ni pamoja na Ferdinand Makaranga, Jonathan Mhagama na Yassin Abdallah.
Kocha Mkuu wa timu ya Uchukuzi, Mputa Zenno alisema wameshindwa kufanya vyema kwenye michuano hiyo kutokana na kuwa na majeruhi wengi.

“Tumekuwa na majeruhi wengi kutokana na wachezaji wetu wengi wamekuwa wakifanya mazoezi baada ya kusikia mashindano fulani, jambo ambalo linasababisha kutokua fiti kwa muda mrefu, hivyo natoa wito waendelee na mazoezi hata kama mashindano yameisha,” alisema Mputa.


Naye kocha mkuu wa GGM, Mikidadi Mbaruku alisema mchezo wa mshindi wa tatu ulikuwa mzuri na mashindano kwa ujumla hayakuwa mazuri kutokana na kushirikisha timu chache, ambazo hazikutoa ushindani mkubwa.
Kwa upande wa Uchukuzi waliopata ni pamoja na David Kunambi, Ramadhani Madebe, Karim Sabu, Seleman Kaitaba na Abubakar Hamis, huku waliokosa kwa kupaisha juu na kipa kudaka ni Erick Mpunga, Issack Ibrahim, Ally Poloto na Said Chembela.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume, timu ya Uchukuzi ilitwaa ubingwa baada ya kuwavuta Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa mivuto 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU). Nayo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) walivutana na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) na kushinda mivuto 2-0.

No comments