MWANTIKA AANZA MAZOEZI RASMI

BEKI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, David Mwantika, ameanza rasmi mazoezi ya wenzake wiki hii ikiwa baada ya kuugua ghafla uwanjani wiki tatu zilizopita.
Mwantika alipata hitilafu hiyo ya mwili dakika ya 65 wakati Azam FC ikicheza hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mbagala Zakhem na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke, na baadaye ile ya Rufaa ya Muhimbili (MNH).
Baada ya kuhamishiwa Muhimbili na kutibiwa vema kabisa, iliwalazimu madaktari wa hospitali hiyo kumhamishia kitengo cha magonjwa ya moyo cha Taasisi ya Jakaya Kikwete na kufanyiwa vipimo ili kujua kama ana tatizo la aina hiyo.
Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa tayari wamepokea majibu ya vipimo hivyo vinavyoonyesha kuwa beki huyo hana tatizo la moyo akidai yupo fiti kabisa na ndio maana wamemruhusu kuanza mazoezi mepesi.
“Mwantika alipata huduma Muhimbili na akalazwa katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete na baada ya kufanyika uchunguzi wa kina kabisa na vipimo vya kina na kuangalia mishipa ya damu ya moyo imethibitika kwamba Mwantika hana tatizo la moyo.
“Na sasa amerudi tena na katika siku mbili hizi tulianza kuangalia uwezo wake wa kukimbia na uwezo wake wa pumzi kwa hiyo alianza mazoezi ya kukimbia kwa dakika 20, dakika 30 na leo (jana) amekimbia dakika 45,” alisema.
Mwankemwa alisema kuwa wiki ijayo beki huyo ataruhusiwa kuanza mazoezi ya kawaida na wenzake tayari kabisa kurejea katika ushindani.
Chanzo,Mtandao wa Azam FC.

No comments