MECHI YA MTIBWA SUGAR NA AZAM FC KUCHEZWA SAA 10 JIONI
Mabingwa wa ligi kuu bara mara mbili, Mtibwa Sugar Sports Club, kesho (Jumamosi) wana tam tam watashuka dimbani kuwakabili Azam fc katika mchezo wa ligi kuu bara (Vodacom Premier League).
Mchezo huo wa ligi kuu bara (Vodacom Premier League) utaanza kuchezwa majira ya saa 10:00 jioni katika dimba la Manungu Complex, awali mchezo huo ulikuwa uchezwe saa 8:00 kamili mchana.
Mtendaji wa klabu ya Mtibwa Sugar Sports Club Swaburi Abubakary ameeleza kuwa mechi hiyo sasa itachezwa saa 10 kamili jioni baada ya kupata maelezo kutoka bodi ya ligi.
"Ni kweli tumepokea taarifa hiyo, mchezo utachezwa kesho (Jumamosi) majira ya saa kumi jioni, awali mchezo huo ulikuwa uchezwe mchana, tunawaomba mashabiki waje kwa wingi watupe support” alisema Swaburi Abubakar.
Kikosi cha Mtibwa Sugar kimezidi kuimarika baada ya wachezaji wake tegemeo Salum Kupela Kanoni “Mbavu kunesa” na Issa Rashid “Baba Ubaya” kupona, wachezaji wote wawili walikuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu na sasa wamepona wako salama kuendelea kutumikia kikosi cha Mtibwa Sugar.
Salum Kanoni aliumia katika mchezo wa kombe la shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Buseresere huku Issa Rashid yeye akipata majeraha ya goti katika mchezo wa ligi kuu bara dhidi ya Mwadui katika mchezo uliochezwe Mwadui Complex.
Kwa upande mwingine kikosi cha wana tam tam kitaendelea kukosa huduma ya Hassan Mganga anayesumbuliwa na maumivu ya goti ambayo aliyapata katika mchezo wa kombe la shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Stand United na mchezaji mwingine ni Stamil Mbonde ambaye anasumbuliwa na malaria.
Post a Comment