AZAM FC KUWAFUATA SINGIDA UNITED DODOMA

Kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kesho Jumatano alfajiri kuelekea mkoani Dodoma, tayari kabisa kwenda kuivaa Singida United.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) unatarajia kufanyika Jumamosi hii Septemba 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri saa 10.00 jioni.
Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa ya NMB na Tradegents, inaelekea huko ikiwa na morali kubwa kutokana na mwenendo mzuri waliokuwa nao kwenye ligi hiyo.
Hadi sasa ikiwa ndio timu pekee ambayo haijaruhusu wavu wake kuguswa, imecheza mechi nne za ligi na kujikusanyia pointi 10 katika nafasi ya pili kwenye msimamo sawa na Mtibwa Sugar iliyo kileleni, ikizidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga.
Singida United yenyewe ipo nafasi ya tatu kwa pointi tisa ilizojikusanyia baada ya kushinda mechi tatu na kufungwa mchezo mmoja.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali na wa aina yake kutokana na mwenendo mzuri wa vikosi vyote viwili, lakini Azam FC ikionekana kuimarika zaidi kiuchezaji mechi hadi mechi jambo ambalo limeifanya kuwa timu isiyofungika hadi sasa.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, ameweka wazi kuwa kuelekea mchezo huo wanatarajia kulifanyia kazi tatizo la ufungaji kwenye kikosi hicho baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi katika mchezo uliopita.
Kuelekea mtanange huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza mazoezi leo Jumatatu jioni ndani ya viunga vyake vya Azam Complex baada ya mapumziko ya jana.

No comments