YAHAYA MOHAMED ATAMBA KUIFANYIA MAKUBWA AZAM FC
Mchezaji mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati Azam FC, Yahaya Mohammed, amesema kuwa amejiunga na timu hiyo
kwa kazi moja tu kuipigania timu ili kupata matokeo bora uwanjani.
Mohammed
jana jioni alikamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo akisaini mkataba wa
miaka miwili tayari kabisa kuitumikia Azam FC kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL), Kombe la Kagame ikiwa kama bingwa mtetezi, Kombe la
Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Mshambuliaji
huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, 28, amesema mashabiki wa Azam FC wakae
mkao wa kufurahi kwani kwa kushirikiana na wachezaji wenzake watafanikiwa
kuwapa furaha kwa kupata matokeo bora uwanjani.
“Ninafuraha
kubwa kusaini mkataba wa kujiunga na Azam FC, nimejipanga kukabiliana na
changamoto zote hapa kwani ukiwa mchezaji ni kazi yako na unapaswa kujiandaa na
hilo na kila muda unapaswa kujiandaa na kazi yako,” alisema.
Staa
huyo pia alichukua fursa hiyo kuomba sapoti kwa mashabiki wa timu hiyo,
waendelee kuisapoti Azam FC kwani hilo litawapa nguvu wao kama wachezaji kuweza
kufanya vizuri uwanjani na kupambana kwa ajili ya matokeo bora.
“Tunahitaji
sapoti yao na waendelee kuipa sapoti Azam FC, hilo litatufanya sisi kuipeleka
timu mbele zaidi, sisi pekee wachezaji hatuwezi kuipeleka timu mbele kama
mashabiki hawatusapoti, tunawahitaji sana na sisi wanatuhitaji, waisapoti timu
katika hali mbaya na nzuri kwani hii ni timu yao, sisi tutaingia uwanjani
kucheza kwa ajili yao na tunawaahidi tutawapa furaha kwa matokeo mazuri,”
alisema.
Akizungumzia
kuhusu soka la Tanzania, aliongeza kuwa: “Kwa sasa sijui lolote kuhusu soka la
Tanzania kwani nikiwa Ghana hakuna kituo cha televisheni kinachoonesha ligi ya
hapa, ila kwa sasa mimi ni mwanafamilia wa Azam FC, hilo sio tatizo kwangu
ukiwa kama mchezaji unatakiwa kusimama popote na kucheza na kufanya vizuri kwa
ajili ya klabu.”
Straika
huyo anatarajia kuanza rasmi mazoezi Desemba 3 mwaka huu, wakati kikosi hicho
kitakaporejea kutoka likizo ya wiki mbili, ambapo kesho Ijumaa atarejea nchini
kwao Ghana kwa ajili ya kujipanga zaidi pamoja na mapumziko mafupi.
Mbali na
kuiongoza Aduana Stars kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya
Ghana msimu uliopita, Mohammed pia aliiibuka mfungaji bora namba mbili wa ligi
hiyo kwa mabao 15 aliyofunga nyuma ya Latif Blessing wa Liberty Proffesional
aliyetupia 17.
Mohammed alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana
kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN)
zilizofanyika mwaka juzi nchini Afrika Kusini na timu hiyo kuwa washindi wa
pili akiwa pamoja na straika mwingine aliyesajiliwa na Azam FC, Samuel Afful.
Post a Comment