FKF WALAUMU HALI YA KISIASA NCHINI KENYA
Wizara ya michezo na shirikisho la soka nchini Kenya wamelaumu hali ya kisiasa nchini humo kuwa sababu ya nchi hiyo kukosa nafasi ya uandaaji wa fainali za CHAN mwaka 2018.
Katibu wa kudumu katika Wizara hiyo Peter Kaberia amesema kuwa viongozi wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF waliwaambia kuwa hawakuwa na tatizo la maandalizi ila tatizo lilikuwa ni hali ya kisiasa nchini.
Kaberia ameongeza kuwa hatua hiyo imewapa huzuni pamoja na kwamba viwanja viwili vilikuwa tayari kuandaa michuano hiyo ya CHAN na maandalizi yalikuwa yanakwenda vizuri.
Kenya bado ipo kwenye mvutano wa kisiasa kuhusu Uchaguzi wa urais ulipangwa kufanyika tarehe 26 mwezi Oktoba.
Naye rais wa Shirikisho la soka nchini humo Nick Mwendwa amesisitiza kauli iliyotolewa na afisa wa serikali kuwa sababu ya kisiasa ndio iliyokuwa kikwazi cha Kenya kupoteza nafasi hiyo.
Aidha, amesema kuwa uongozi CAF imewahakikishia kuwa itawaunga katika mpango wa Kenya kuomba nafasi ya kuandaa fainali ya kombe la dunia kwa vijana wasiozidi miaka 17 au 20 mwaka 2019.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kufanikisha hilo, ni lazima viwanja vinne vijengwe na kukamilika kufikia mwezi Februari mwaka 2018.
Uongozi wa CAF ulifanya maamuzi ya kuipokonya Kenya nafasi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kutoa sababu tatu muhimu.
Kwanza ikiwa ni maandalizi ya ukarabati na ujenzi wa viwanja kwenda taratibu, viongozi wa soka kutokuwa wakweli kuhusu maandalizi hayo na mwisho hali ya kisiasa nchini humo.
Mashabiki wa soka nchini Kenya, wameonesha masikitiko makubwa kwa nchi yao kukosa nafasi hii ya kipekee.
Mwaka 1996, Kenya ilikosa nafasi kama hii ya kuandaa fainali ya mataifa bingwa barani Afrika kutokana na sababu kama hizi lakini pia mizozo kati ya viongozi wa soka nchini humo.
Post a Comment