ENOCK ATTA ATAMBA KUIPA MATAJI AZAM FC


Ninafuraha kubwa kuwa hapa, nimekuja kushinda makombe pamoja na kuweka historia hapa kabla sijaondoka, nimejiandaa kuzikabili changamoto zote zilizopo mbele yangu,” hiyo ndio kauli ya kwanza ya nyota mpya wa Azam FC, Enock Atta Agyei, alipofanya mahojiano maalumu na www.azamfc.co.tz.
Agyei, 17, ametua Azam FC akitokea Medeama ya Ghana baada ya kulivutia benchi jipya la ufundi la timu hiyo chini ya Zeben Hernandez, wakimshuhudia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Waghana hao wakivaana na Yanga (1-1) katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tayari nyota huyo ameshasaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia mabingwa hao akipewa jezi namba 10, ambapo jana aliweza kuanza rasmi mazoezi na wachezaji wenzake huku akionekana kuwafurahisha zaidi makocha kwenye mazoezi hayo.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, imemchukua kinda huyo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kitaifa na Kimataifa msimu ujao.
Maisha mapya Azam FC
Licha ya Agyei kusumbuliwa na joto la jijini Dar es Salaam tofauti na hali ya hewa aliyoizoea ya joto kiasi nchini Ghana, nyota huyo amefurahishwa na mazingira aliyoyakuta Azam FC.
“Ninafuraha kubwa kujiunga na Azam FC, najisikia nipo nyumbani kiukweli, siijui Azam lakini nimefanya uchunguzi kupitia mitandao na kuijua vema, inacheza soka zuri na pia wako vizuri, naamini tutafikia mafanikio,” alisema.
Tanzania vs Ghana
Kwa siku chache alizokuwa nchini hapa, Agyei amesema kuwa moja ya utofauti mkubwa wa soka la Tanzania na Ghana ni namna ya uchezaji, Ghana wakicheza soka la kumiliki mpira na nguvu tofauti na Tanzania huku akidai kuwa aina yao ya uchezaji ndio iliyofanya wakapata matokeo bora dhidi ya Yanga.
“Ni vizuri kwangu kuwa hapa, bado sijalijua sana soka la hapa, najua soka la Ghana lipo juu kuliko hapa, lakini unapokuwa mchezaji unahitaji kubadilisha mazingira, unatakiwa kuhama timu bila kujali nini kitatokea na cha muhimu ni kupambana wewe mwenyewe kwa kufanya kazi kwa bidii,” alisema.
Kauli kwa mashabiki
Nyota huyo wa zamani wa Windy, anajua kiu waliyokuwa nayo mashabiki wa Azam FC kutoka kwake, ambapo amewaahidi kuwapa mambo mazuri bila kuwaangusha.
“Najua timu ilinifuatilia, napenda kuwaambia tayari nipo hapa, nawaheshimu na nawaahidi mazuri, watarajie vitu tofauti na sitawaangusha hata kidogo kiukweli, nitahakikisha nashirikiana vema na wenzangu na kufanya kila kitu kama timu na hatimaye kupata mafanikio msimu ujao,” alisema
Ndoto za kuitwa Black Stars
Agyei alisema kuwa ana mahusiano mazuri na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’, Avram Grant na kudai kabla hajaondoka alimuahidi kumfuatilia wakati atakakapokuwa anaichezea Azam FC.
“Nina ndoto kubwa sana za kuitwa timu ya Taifa tokea nipo mdogo, na ndio maana katika historia zangu nimejitahidi kutafuta uzoefu kwa kuchezea timu tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na kufanya kazi yangu kwa bidii.
“Najua hivi sasa niko hapa sitaki kusema itanichukua muda gani kuitwa timu ya Taifa lakini naamini ndani ya mwaka huu nitakuwa nimeitwa, Grant atakuwa akinifuatilia nimeambiwa na viongozi wangu wa zamani wa Medeama kuwa Grant ameanza kunifuatilia, aliziomba DVD zangu zote nilizoichezea timu hiyo kwenye michuano ya CAF,” alisema.  
Zilizokuwa zikimfukuzia
Kama si uharaka wa viongozi wa Azam FC walioamua kufunga safari hadi Ghana kunasa saini yake kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, basi huenda kinda huyo angesajiliwa na timu nyingine kwa mujibu wa maelezo yake.
“Nakumbuka nilianza kufuatwa na uongozi wa Azam FC mara baada ya kucheza na Yanga kule Ghana, tulikubaliana kila kitu pamoja na uongozi wa Medeama, ila ulipomalizika mchezo wetu ule kuna watu wanaotokea Yanga nao walinifuata na kuniambia wanataka kunisajili, lakini niliwakatalia na kuwaambia natakiwa kuja hapa (Azam FC),” alisema.
Aliyemvuta kuwa mwanasoka
Kinda huyo hatamsahau Baba yake mzazi, Owusu Nkwantabisa, ambaye kwa kiasi kikubwa ndiye aliyempelekea leo hii kuwa mwanasoka kutokana na kumlea kwenye mazingira ya mchezo huo wakati huo yeye akiwa kama kocha.
“Baba yangu ndiye amenifanya mimi kucheza mpira leo hii, alihakikisha nipo sehemu nzuri, yeye alikuwa ni kocha wa timu za madaraja ya chini, hakuwahi kufundisha soka la kulipwa, amewahi kufundisha magwiji wengi wa Ghana akiwemo Charles Amoah, kiukweli ni Baba wa ukweli na Mwanamume bora, nampenda sana,” alisema.
Mipango yake Ulaya
Alisema kuwa ndoto yake ni siku moja kucheza Ulaya, lakini amedai si lazima sana akacheze huko ili afanikiwe bali hata hapa Afrika panatosha kumfanya awe na maisha bora cha msingi ni yeye kufanya kazi kwa bidii.
“Kila mchezaji anaheshimu kucheza soka Ulaya, hii ni kutokana unapocheza Ulaya unaweza kutatua matatizo yako mengi kwenye maisha, hayo ni kwa mujibu wa maneno ya watu, lakini mimi naamini ya kuwa popote panaweza kuwa Ulaya inategemeana na wewe unaifanyaje kazi yako.
“Mtu anayefanya kazi kwa bidii akiwa kijijini anaweza kujenga nyumba, hata mtu wa mjini vilevile hivyo haijalishi kuwa lazima uwe Ulaya ndio ufanye hivyo, lakini unaweza kuwa Afrika na kufanikisha hilo kama upo makini na unafanya kazi yako kwa bidii,” alisema.
Aina ya uchezaji
Atta Agyei ambaye amejaliwa mbinu na uwezo mkubwa wa kupiga pasi zenye jicho. Kiasili anacheza winga zote mbili za kulia na kushoto, lakini anatumia zaidi kwa ufasaha mguu wake wa kushoto, huku ule wa kulia akiutumia kidogo kidogo.
Kiuchezaji uwanjani anavutiwa na staa wa Brazil, Givanildo Vieira de Sousa maarufu kama Hulk, akidai kuwa anavutiwa naye kutokana na staili zao za uchezaji kufanana wote wakicheza kwa kutumia nguvu, akili na uwezo wa kupambana uwanjani kuwania mipira, kupiga mashuti na kufunga mabao.
Staili ya maisha
Unaweza kushangaa, lakini Agyei anajitofautisha na aina ya wachezaji wengi duniani kutokana na utamaduni wa masiha yake ya soka aliyojiwekea, ambao ni kutumia muda mwingi kupumzika zaidi huku akiwa sio mtu wa kujirusha.
“Mimi sipendi kujirusha kwenye starehe, mimi huwa na vitu viwili vikubwa, kufanya mazoezi na kisha narejea chumbani kwangu kupumzika na kuuweka mwili safi, starehe zinapoteza sana muda na hakuna kitu unachoingiza baada ya kwenda kwenye mambo hayo, mimi ni kazi tu,” alisema.
Agyei alisema wakati wa mapumziko yake hupendelea sana kusikiliza miziki ya dini (gospel), ambayo ndiyo humvutia zaidi huku chakula chake kikuu kikiwa ni wali, maharage na samaki.
Wasifu wake
Enock Atta Agyei alianza kuonyesha kipaji chake akiwa na umri wa miaka sita tu, akianzia kucheza katika timu ya vijana ya King Solomon inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Ghana mwaka 2005.
Kipaji chake kikubwa cha kusakata mpira, kilimfanya akibebe kikosi cha Shule ya Msingi Effiduase Presby aliyokuwa akisoma, ambacho kilifuzu ngazi ya kanda na baadaye mkoa katika michuano ya shule nchini humo.
Mara baada ya michuano hiyo, Agyei alikuwa ni miongoni mwa nyota 26 waliochaguliwa kujiunga na Chuo cha Taifa Michezo nchini humo, wote wakipendekezwa kuingia katika academy ya chuo hicho.
Kujitoa kwake na kufanya kazi kwa bidii kulimfanya apandishwe haraka kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka 12 hadi 17 kabla hajajiunga na Windy Professionals.
Nyota ya kinda huyo ilizidi kung’ara mwaka jana wakati alipoichezea msimu wa mwisho Windy Professionals na hii ni baada ya kuchangia mabao 24 yaliyofungwa na timu hiyo msimu uliopita, akifunga mwenyewe 17 na kutoa pasi za mwisho saba ndani ya mechi 29 alizocheza.
Mafanikio yake hayo yalimfanya azawadiwe Tuzo ya Mchezaji Bora anayetabiriwa kutikisa baadaye (GN Bank Award), hii ikiwa ni kwa msimu 2015-2016  wa Ligi Daraja la Kwanza Ghana wakati akiichezea Windy.
Desemba mwaka jana, haikushtua kusikia Medeama FC ya huko ikinasa saini yake, ambayo amefanikiwa kuiongoza kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya wiki iliyopita kutua Azam FC.
Kinda huyo mbali na kutokuwa na uzoefu wa mikikimikiki ya Ligi Kuu, tayari ameshawahi kuitwa katika timu za Taifa za vijana za Ghana, akianzia ya chini ya miaka 17 na sasa akiwa kwenye kile cha chini ya miaka 20.
Licha ya kutocheza hata mechi moja mpaka sasa akiwa na U-20 ya Ghana, Agyei alikuwemo katika kikosi cha timu hiyo kilichotolewa na Senegal kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye mechi za kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wa umri huo zitakazofanyika Zambia mwakani.

No comments