AZAM FC YAMALIZA KAMBI VISIWANI ZANZIBAR KWA USHINDI MWEMBAMBA
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, usiku wa kuamka leo imemaliza kambi ya Zanzibar kwa kuichapa timu ya Taifa ya Jang’ombe bao 1-0 kwenye mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu ujao.
Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Amaan ni wa pili kwa Azam FC kwenye kambi ya Zanzibar baada ya ule wa kwanza uliofanyika Jumatano iliyopita kuisha kwa ushindi mwingine wa bao 1-0, lililofungwa na Fuadi Ndayisenga aliyeko katika majaribio.
Iliichukua dakika ya tano tu ya mchezo kwa Azam FC kuweza kuandika bao hilo pekee, likifungwa na Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyepokea pasi safi ya Michael Bolou na kuwachomoka mabeki wakidhani ameotea kabla ya kumchambua kipa wa Jang’ombe, Ahmed Seleman na kutupia mpira wavuni.
Azam FC iliweza kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa wapinzani wao, lakini tatizo kubwa lililoonekana ni upotezaji wa nafasi nyingi za kufunga mabao na kikwazo kingine kikiwa ni safu ngumu ya ulinzi ya Jang’ombe.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa bao hilo moja, ambapo Kocha Mkuu Zeben Hernandez, aliweza kubadilisha wachezaji nane kilipoanza kipindi cha pili lengo likiwa ni kuwatathimini zaidi wachezaji wake wote.
Walioingia kipindi cha pili ni mabeki Ismail Gambo na Gadiel Michael, viungo Mudathir Yahya, Masoud Abdallah, Salum Abubakar, washambuliaji Brian Abbas, Ibrahima Fofana na Fuadi Ndayisenga, huku waliotoka wakiwa ni David Mwantika, Bruce Kangwa, Himid Mao, Bolou, Mcha, Frank Domayo, Bocco na Ramadhan Singano.
Jang’ombe walionekana kucheza vema kipindi cha pili tofauti na kipindi cha kwanza, jambo ambalo liliipa wakati mgumu Azam FC licha ya kufanya mabadiliko hayo.
Safu ya ushambuliaji ya Azam FC iliyokuwa ikiundwa na Fofana, Ndayisenga, Abbas kipindi cha pili, itabidi ijilaumu yenyewe baada ya kukosa mabao mengi ya wazi wakiwa ndani ya eneo la 18, ambayo yangeweza kuwapa ushindi mnono mabingwa hao.
Mara baada ya Azam FC kumaliza ziara yake hiyo, kesho Jumapili saa 3 asubuhi inatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na programu yake ya maandalizi ya msimu ujao.
Kikosi Azam FC
Aishi Manula, Bruce Kangwa/Gadiel Michael dk 46, David Mwantika/Ismail Gambo dk 46, Aggrey Morris, Jean Mugiraneza, Himid Mao/Masoud Abdallah dk 46, Michael Bolou/Mudathir Yahya dk 46, Frank Domayo/Salum Abubakar dk 46, Khamis Mcha/Fuadi Ndayisenga dk 46, John Bocco (C)/Ibrahima Fofana dk 46, Ramadhan Singano/Brian Abbas dk 46
Post a Comment