PONDAMALI, MANYIKA DARASANI TFF
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefanikiwa tena. Safari FIFA - Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu limeipa nafasi Tanzania kuwapa mafunzo ya juu ya
ukocha wa makipa (Advanced Goalkeeping Coach Course) ikiandika historia kuwa
nchi ya pili barani Afrika kwa makocha wa nafasi hiyo baada ya Botswana.
Makocha wa
makipa 25 hususani wa wa timu za taifa, timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, wanahudhuria kozi hiyo inayoongozwa na Alejandro Heredia ambaye
ni Mkufunzi kutoka FIFA.
Makocha hao ni
Peter Manyika (Taifa Stars ya Tanzania), Saleh Ahmed (Zanzibar Heroes); Muharami
Mohammed (Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 - Serengeti
Boys); Mohammed Silima (Timu ya Taifa ya Vijana Zanzibar) na Elyutery Mhoery
(Timu ya Taifa ya Wanawake - Twiga Stars) na msaidizi wake ambaye pia anachezea
JKT Queens, Fatuma Omary.
Wengine ni
makocha maarufu wa makipa wakiwamo Juma Pondamali (Young Africans); John Bosco
(Majimaji ya Songea); Salimu Tupa (Tanga); Bakari Ali Hamadi (Wete Pemba –
Zanzibar); Hafidh Muhidin Mcha (Mkoani Pemba – Zanzibar); Mussa Wanena (Kagera
Sugar); Juma Bomba (African Lyon), Adam Abdallah Moshi (Simba SC), Idd
Mwinchumu (Azam FC) na Hussein Tade (Seeb Club-Oman/Toto African).
Pia wamo Khalid
Adams (Mwadui FC); Josia Steven (Mbeya City); Herry Boymanda (Tanzania
Prisons); Emmanuel Mwansile (Polisi Morogoro); Ben Kalama (Stand United);
Abdallah Said (JKT Ruvu); Patrick Mwangata (Mtibwa Sugar); Augustin Malindi
(Mkoa wa Kigoma); Raphael Mpangala (Ndanda FC); Salimu Tupa (Tanga) na nAbdul
Mgude (Coastal Union ya Tanga).
“Mjione kwamba
mmepewa kipaumbele,” alisema Heredia akiwanoa makocha hao na kuongeza:
“Kinachohitajika sasa ni juhudi tu. Kozi hii haijafanyika pengine hapa barani
Afrika zaidi ya Botswana. Mjue kuwa mna bahati.”
Akitoa nasaha
wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo, Makamu Rais wa TFF, Wallace Karia aliishukuru
FIFA na CAF kwa namna inavyoshirikiana na TFF katika kuwapa kozio nyingi za
makocha wa timu kwa wachezaji wa mbele, makocha wa makipa na waamuzi wa
madaraja tofauti.
“Hakuna
kipindi TFF imepata kozi za makocha nyingi za makocha kama kipindi hiki cha
uongozi wa Jamal Malinzi,” anasema Karia na kuongeza: “Tumetoka kwenye kozi ya
makocha wa Daraja A sasa tuko kwenu. Lengo ni Tanzania kuwe na makipa wazuri.
Ninyi mtaleta makipa wazuri. Na hii ni kwa manufaa ya sasa na baadaye kwa
upende wetu, timu zetu na taifa kwa ujumla.”
Karia aliwatia
hamasa makocha hao wanaoshiriki kozi hiyo kuwa, mara baada ya kozi hiyo ipo
siku watakwenda kuwa wakufunzi nje ya mipaka ya nchi kadhalika makocha ambao
wanaweza kupata kazi mahala popote duniani hasa ukizingatia walimu wa daraja
lao wako Tanzania na Botswana tu.
Kadhalika,
Makamu huyo wa Rais wa TFF alielezea kuwa mpira wa miguu una changamoto nyingi
na nyingine husababishwa na watalaamu hao kubweteka kwa mafanikio. “Hili ni
tatizo. Tubadilike kifikra na kivitendo. Msilaze damu, kuweni active (mahiri).”
Post a Comment