LIGI YA WANAWAKE KUANZIA NOVEMBA 26

Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Novemba 26, 2017 katika vituo viwili vya Dar es Salaam na Arusha, imefahamika.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi amesema Kundi A litakuwa Dar es Salaam na timu za Simba Queens ya jijini Dar Es Salaam iliyopanda daraja msimu huu.
Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Mburahati Queens, JKT Queens, Evergreen zote za Dar es Salaam pamoja na timu za Fair Play ya Tanga na mabingwa watetezi – Mlandizi Queens.
Kundi B litakuwa na timu za Alliance ya Mwanza ambayo imepanda kutoka kituo cha Dodoma. Timu nyingine ni Marsh Academy pia ya Mwanza; Panama ya Iringa; Kigoma Sisterz ya Kigoma, Baobab ya Dodoma na Majengo Queens ya Singida.
Time hizo zitapambana katika vituo hadi Desemba 9, mwaka huu kabla ya kutoa jumla ya timu nane kwa maana ya nne kutoka kila kundi. Timu hizo nane zitapambana katika hatua ya Nane Bora ya Ligi hiyo kuelekea ubingwa. Ligi inatarajiwa kumalizika Machi 28, mwakani.
Kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, TFF imetoa kalenda ya mashindano hayo ambako usajili utakuwa kati ya Oktoba 25 na Novemba 10, mwaka huu.
Novemba 12 hadi 17, mwaka huu ni kipindi cha pingamizi  wakati Novemba 18, mwaka huu kutakuwa na kikao cha  Kamati ya Sheria kabla ya Novemba 20, mwaka huu kutoa leseni za wachezaji.
Novemba 24, mwaka huu kutakuwa na Semina ya Viongozi wa klabu, Waamuzi na Makamishna jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumalizika hatua ya makundi Desemba 9, mwaka huu Ligi Kuu hatua ya Nane Bora ‘Super 8’ itaanza Desemba 20, mwaka huu.

No comments