KOCHA AZAM FC AWAAMBIA MASHABIKI WASIWE NA HOFU

KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kuwa timu itaimarika na kupata matokeo bora msimu ujao.
Kauli hiyo imekuja saa chache mara baada ya kikosi hicho kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Njombe Mji, kwenye mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu ujao uliofanyika Uwanja wa Amani, Makambako jana jioni.
Kocha huyo raia wa Romania alibadilisha kikosi chote kilichocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City isipokuwa beki David Mwantika, kilichosheheni wachezaji wengi wapya vijana kabla ya kipindi cha pili kuabadilisha tena kwa kukiingiza kikosi kingine cha wachezaji wakongwe.
“Ligi ya hapa inaanza baada ya mwezi mmoja na mashabiki wanatakiwa kuelewa ya kuwa matokeo haya hayamaanishi chochote, bado tupo kwenye kipindi cha maandalizi na timu itafanya vizuri msimu ujao cha muhimu ni mshabiki kuendelea kuisapoti timu,” alisema Cioaba wakati akizungumza na mtandao wa klabuwww.azamfc.co.tz
Alisema aliwatumia kikosi kingine cha wachezaji vijana katika mchezo huo ili kuwafahamu wachezaji wake na watu kujonea Azam FC inatarajia kuvuna nini kwa siku za baadaye, kama mikakati aliyojiwekea katika mechi za Nyanda za Juu Kusini 
“Leo (jana) nilifanya mabadiliko kwa kuwachezesha wachezaji vijana waliopandishwa na baadhi ya wachezaji wapya, ili kuona kitu gani kinaweza kutokea hapo baadaye, kuona viwango vyao, wengi walizoea kucheza kwenye kiwanja cha nyasi bandia pale Azam Complex, hawakuwahi kucheza katika kiwanja kama hiki.
“Kama kocha nimejaribu kuwatumia wachezaji wote niliokuwa nao hapa, nikisharejea Chamazi baada ya mechi hizi nitapitisha orodha ya mwisho ya wachezaji wangu wa msimu ujao,” alisema.
Alisema: “Nitaendelea programu yangu ya mazoezi huku na sitaangalia matokeo baada ya kurejea nyumbani na wachezaji wote wa timu ya Taifa watakaporejea na kufanya nao mazoezi kwa pamoja, Daniel, Stephan, Himid, Mahundi, Shaaban, Mbaraka, Salmin na wachezaji wengine wapya wawili na kuwafanyisha mazoezi ya kiufundi pamoja na kuijenga timu, kwa mashabiki wa kweli nawapa ujumbe kuwa timu hii itakuwa na matokeo mazuri.”
Cioaba alisema kuwa kwa sasa ni muda wa kuwarekebisha wachezaji wote kwa ajili ya msimu ujao na kudai mashabiki wanatakiwa kuwa na uvumilivu na kuwapa sapoti wachezaji wote waliokuwa kwenye timu.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora ya NMB na Maji safi ya Uhai yaliyokuja na muonekano mpya, leo asubuhi imeanza safari ya kuelekea mkoani Iringa kucheza mchezo mwingine wa kirafiki wa kuhitimisha ziara ya Nyanda za Juu Kusini, utakaofanyika Uwanja wa Samora kesho Jumatano.

No comments